Na Ibrahim Rojala - Geita.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Jimbo la Geita,Neema Chozaile, anayekabiliwa na tuhuma za kupanga njama za kuua maofisa wa Polisi, amesomewa mashtaka mapya ya ugaidi katika Mahakama kuu, Masjala Ndogo ya Geita.
Aidha kesi ya awali namba 16032 ya mwaka 2026, iliyotarajiwa kusikilizwa leo Agosti 10, 2026 katika Mahakama ya wilaya ya Geita majira yasaa sita mchana chini ya Hakimu mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Geita, Mujuni Muchunguzi, ilitajwa saa tatu na robo asubuhi ambapo kiongozi huyo alisomewa shtaka hilo bila ya uwepo wa viongozi wa CHADEMA kutokana na kutofautiana kwa ratiba ya usikilizwaji wake.
Katika shauri hilo Neema alikuwa anatetewa na Wakili Erick Korogo, huku upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili Mkuu, Martha Mwadenya na Wakili Liberatus John ambaye alipopata nafasi ya kuzungumza nje ya Mahakama, amesema licha ya upande wa Jamhuri kudai upelelezi umekamilika, uliomba shauri kusogezwa mbele kwakuwa walikuwa hawajawasilisha taarifa za shauri hilo Mahakama Kuu.

"Tulivyofika mahakamani upande wa Serikali walisema hawaja 'file' shtaka mahakama kuu kwasababu Mahakama ya Wilaya haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo" amesema Wakili Korogo.
Baada ya maombi hayo ya Jamhuri,Hakimu anayesikiliza kesi hiyo,alikubali maombi na kupanga Agosti 14, 2026 ambapo shauri hilo lilipangwa kusikilizwa tena,huku Jamhuri wakitwakiwa kuwasilisha taarifa hizo mahakama kuu.
Hata hivyo, wakati Neema akitoka Mahakamani akiwa ameambatana na Wakili wake, alikamatwa na maofisa wa polisi ambao baadhi walikuwa na sare huku wengine wawili wakiwa wamevaa suti nyeusi ambao walimuingiza kwenye gari aina ya Toyota IST lenye rangi nyeupe na kuondoka naye.
Aidha Wakili wa utetezi Korogo amesema kuwa, mteja wake amesomewa shtaka ya ugaidi bila yeye kuwepo kwakuwa alipewa taraifa baada ya shauri kufunguliwa, kufuatia taharuki hiyo,viongozi wa CHADEMA wakiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Geita, Charles Makanji, walielekeza jeshi la Polisi kufuatilia alipo kiongozi huyo.
Akizungumzia hali ilivyokuwa,Makanji amesema walipofika kwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, Safia Jongo, walielezwa kuwa Neema alikuwa akishikiliwa kwenye kituo kidogo cha Polisi(selo), katika Mahakama kuu, waliporejea mahakamani, walishangazwa kupewa taarifa kuwa kiongozi huyo alikuwa amesomewa mashtaka ya kujihusisha na vitendo vya ugaidi.
"Tumekuja Mahakama ya wilaya tumekuta Neema amesomewa shtaka la ugaidi,hapa tunasubili kumpelekea mahitaji yake walau aende gerezani akiwa amekula," amesema Makanji.
Kutokana na kesi ya ugaidi kutokuwa na dhamana kisheria, Chozaile amepelekwa Gerezani hadi Agosti 14, 2026 atakapofikishwa mahakamani kwa shauri la awali la kula njama ya kuua maofisa wa Polisi.
Pia kuhusiana na shauri la ugaidi linalomkabili, Mtuhumiwa Neema anatarajiwa kufikishwa Mahakama Kuu mnamo Agosti 24, 2026.
Discussion
Reader comments
0 contributions