Na Pascal Tuliano, Kaliua - Tabora.
Kichanga kinachokadiriwa kuwa na umri wa miezi minne hadi mitano kimeokotwa kikiwa kimetelekezwa bila uhai katika eneo la Soko la Misufini, Kijiji cha Kaliua Mashariki, Kata ya Kaliua, Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora.
Kaimu Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Kaliua Mashariki, Revina Victor Mwachang'a, amesema ofisi yake ilipokea taarifa kutoka kwa wananchi kuhusu kuokotwa kwa kichanga hicho.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, kuna uwezekano tukio hilo linahusishwa na kitendo cha utoaji mimba, ingawa mtu anayehusika bado hajafahamika.

Baada ya taarifa kutolewa, Jeshi la Polisi Wilaya ya Kaliua lilifika eneo la tukio na kuanza uchunguzi, ili kubaini mazingira ya tukio hilo, ambapo hatua za awali za uchunguzi zilipokamilika waliruhusu kichanga hicho kizikwe.
Wananchi walioshuhudia tukio hilo wameeleza kusikitishwa na hali hiyo, wakisisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu athari za vitendo vinavyohatarisha maisha na umuhimu wa kuzingatia maadili na misingi ya dini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Maendeleo, Amiri Milinga, ametoa wito kwa wanawake na vijana kufanya maamuzi yenye busara wanapoingia katika mahusiano, ili kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza pale ujauzito unapotokea.
Discussion
Reader comments
0 contributions