Ushirikiano wa viongozi na wananchi katika kudumisha usafi wa mazingira umeendelea kupewa kipaumbele katika Manispaa ya Singida, huku wakazi wakihamasishwa kushiriki kikamilifu katika kufanya mji kuwa safi na kulinda afya za jamii.
Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini, Kiaratu, ameongoza zoezi la usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali ya Manispaa hiyo, ikiwemo eneo la Msikiti wa Taqwa, Kata ya Majengo, akisisitiza kuwa usafi ni jukumu la kila mmoja.
Gari la kukusanya taka likibeba taka katika zoezi la usafi Singida Mjini.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Kiaratu amesema ameona ni vyema mji wa Singida uendelee kuwa safi, akieleza kuwa ushirikiano wa wananchi ndio msingi wa kuufanya mji huo kuwa mfano katika usafi na afya bora.
Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini Yagi Kiaratu (Kulia) akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Singida Godwin Gondwe (kushoto) wakishiriki katika zoezi la usafi Singida Mjini.
“Usafi wa mazingira ni jukumu la kila mmoja wetu. Tukishirikiana tutaifanya Singida kuwa mji wa mfano kwa usafi na afya bora kwa wananchi wake,” alisema Kiaratu.
Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini Yagi Kiaratu (wa kwanza) akiwaongoza wananchi katika zoezi la usafi
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, Mkuu wa Wilaya ya Singida, Godwin Gondwe, amewapongeza wananchi waliojitokeza kushiriki zoezi hilo na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kuhamasisha usafi wa mazingira kwa lengo la kulinda afya za wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Singida Godwin Gondwe akishiriki zoezi la usafi Singida Mjini
Kwa upande wao, wananchi wa maeneo hayo wameeleza kufurahishwa na ushiriki wa viongozi wa Manispaa ya Singida katika zoezi hilo, wakisema hatua hiyo imewapa hamasa ya kuendelea kudumisha usafi katika mitaa yao.
Wananchi wa Singida Mjini wakiwa katika zoezi la usafi katika Manispaa ya Singida.
Discussion
Reader comments
0 contributions