Na Saulo Stephen - Singida.
Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini, Yagi Kiaratu ameongoza hafla ya utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa mwaka 2025/2026 iliyofanyika leo Mei 08,2026 katika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida Mkoani Singida.
Hafla hiyo imewakutanisha wanufaika wa Viongozi wa chama na serikali pamoja na maafisa maendeleo ya jamii kata ambapo jumla ya vikundi 25 vilinufaika na mpango huo wa uwezeshaji kiuchumi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mbunge Yagi Kiaratu amevisisitiza vikundi vilivyopata mikopo kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa ili ziweze kuleta maendeleo ya kweli kwa wanufaika pamoja na jamii zao. Aidha, amevitaka wanufaika kuhakikisha wanarejesha mikopo hiyo kwa wakati ili kutoa nafasi kwa vikundi vingine kunufaika na mpango huo muhimu wa serikali.
Mbunge huyo pia ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Singida kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya mikopo ya vikundi maalum, akieleza kuwa hatua hiyo ni utekelezaji mzuri wa sera za serikali za kuwawezesha wananchi kiuchumi. Amesema mikopo hiyo imekuwa msaada mkubwa kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu katika kujikwamua kiuchumi kupitia shughuli mbalimbali za uzalishaji mali.

Awali akiwasilisha taarifa kwa mgeni rasmi kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida, Kaimu Mkurugenzi Upendo Naftali Amesema halmashauri hiyo imeendelea kutekeleza utoaji wa mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa lengo la kuinua hali zao za kiuchumi.
“Halmashauri ya Manispaa ya Singida imeendelea kutoa mikopo inayotokana na asilimia 10 ya fedha za mapato ya ndani kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Katika mwaka 2025/2026 halmashauri ilitenga shilingi 673,754,260 ikiwa ni asilimia 10 ya mapato ya ndani, huku hadi Aprili 2025 kiasi cha shilingi 397,687,584.81 kikiwa kimetengwa kwa ajili ya mikopo hiyo,” alisema Upendo Naftali.

Aidha, Amebainisha kuwa katika kipindi cha Januari hadi Machi 2025 halmashauri ilipokea maombi ya mikopo kutoka vikundi 59.
Discussion
Reader comments
0 contributions