Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kagera, Dkt. Nazir Karamagi, amewaelekeza viongozi wa chama hicho katika ngazi zote kuhakikisha kero na changamoto za wananchi zinakuwa agenda kuu katika vikao vya ndani vya chama, ili ziweze kufanyiwa kazi na kuwasilishwa serikalini kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi.
Dkt. Karamagi amesema maelekezo hayo yanatokana na msimamo wa chama wa kuelekeza nguvu katika kuwahudumia wananchi kwa kuwasikiliza, kubaini kero zao na kuhakikisha zinawakilishwa ipasavyo ndani ya Serikali. Amesema vikao vya chama kuanzia ngazi ya mashina, matawi, kata, wilaya hadi mkoa vinapaswa kujadili changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo yao.

Pamoja na kujadili kero za wananchi, vikao hivyo vinapaswa kuzingatia kalenda ya CCM na kufanyika kwa wakati katika ngazi zote, hatua ambayo amesema itasaidia kuimarisha uhai wa chama na kuongeza uwezo wa viongozi wake katika kuwahudumia wananchi.
Dkt. Karamagi ameyasema hayo baada ya kuhitimisha ziara ya kikazi ya kukutana na Halmashauri Kuu za CCM za wilaya mbalimbali mkoani Kagera, ambapo pia alizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za CCM Mkoa wa Kagera, Manispaa ya Bukoba, kuhusu tathmini na maelekezo ya vikao vivyopita.
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, vikao hivyo pia vilifanya tathmini ya pamoja na kuangalia mafanikio yaliyopatikana mkoani Kagera wakati na baada ya uchaguzi huo, ambapo mkoa uliendelea kuwa salama kutokana na maandalizi yaliyofanywa na chama, ikiwemo mchakato wa uteuzi wa wagombea ambao ulikua ni huru na haki amesema walihakikisha wanaostahili wanachaguliwa.

Aidha, amewataka viongozi na wanachama wa CCM kurejesha umoja miongoni mwao kwa kuondoa tofauti zilizojitokeza wakati wa uchaguzi, akieleza kuwa katika uchaguzi wa ndani wanaoshindana huwa ni wanachama wa chama kimoja. Lakini pia amesema makundi yaliyobaki baada ya uchaguzi yanapaswa kuvunjwa na wanachama kurejea katika mshikamano wa chama.
Suala uhusiano kati ya CCM na Serikali, Dkt. Karamagi amesema mahusiano katika ngazi ya mkoa na wilaya ni mazuri, huku changamoto ndogo zikibainika katika baadhi ya maeneo ya vijiji na vitongoji kutokana na uelewa mdogo wa baadhi ya viongozi kuhusu nafasi na majukumu ya chama na Serikali.
Amesema takribani asilimia 90 ya mahusiano hayo ni mazuri na elimu zaidi itatolewa ili viongozi na wanachama waelewe vizuri mahusiano hayo na kuimarisha uhai wa chama kupitia mabalozi wao.
Kwa upande mwingine, Dkt. Karamagi ameupongeza uongozi wa Serikali mkoani Kagera pamoja na vyombo vya usalama kwa hatua walizochukua kudhibiti viashiria vya uvunjifu wa amani na kuhakikisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 unafanyika katika mazingira ya usalama na amani.
Discussion
Reader comments
0 contributions