Skip to main content

KAZAROHO WAONJA 'MATUNDA' YA UHURU, HAWAKUWA NA MAJI KWA ZAIDI YA MIAKA 90

Na Daniel Gahu – Katavi.

KAZAROHO WAONJA  'MATUNDA' YA UHURU, HAWAKUWA NA MAJI KWA ZAIDI YA MIAKA 90

Na Daniel Gahu – Katavi.

Wananchi wa Kijiji cha Manga, Kitongoji cha Kaza Roho, Kata ya Kasokola, Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi, wameondokana na adha ya ukosefu wa maji iliyodumu kwa zaidi ya miaka 90, baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kisima cha maji safi na salama kilichofadhiliwa na familia ya Al-Marhum Haji Abdulrahman Nkuhi.

Kisima hicho kimekabidhiwa kwa wananchi katika hafla iliyohudhuriwa na Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini, Haidary Hemed Sumry, huku wananchi wakieleza matumaini mapya ya kuboresha afya na maisha yao kutokana na upatikanaji wa huduma hiyo muhimu.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya mradi huo, mfadhili wa kisima hicho, Bi. Fancy Nkuhi, amesema mradi huo umetolewa kama sehemu ya sadaka ya familia yao kwa jamii, kwa lengo la kuwawezesha wananchi kupata huduma ya maji safi na salama.

Amesema aliguswa na hali ya wananchi wa eneo hilo baada ya kuona video fupi iliyoonesha namna walivyokuwa wakihangaika kutafuta maji, jambo lililomsukuma kuamua kutoa sadaka hiyo.

“Niliona changamoto waliyokuwa nayo wananchi hawa na nikaguswa sana. Nikaona ni vyema familia yetu kutoa sadaka ya kisima hiki ili kuwasaidia kupata maji safi na salama,” amesema Bi. Nkuhi.

Bi. Nkuhi amesema furaha yake ni kubwa baada ya kuona namna wananchi walivyoupokea mradi huo, akieleza huku akibubujikwa na machozi ya furaha kutokana na kuona sadaka ya familia yao imeleta mabadiliko ya moja kwa moja katika maisha ya jamii.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini, Haidary Hemed Sumry, amewataka wananchi wa Kijiji cha Manga kuhakikisha kisima hicho kinatunzwa, kinalindwa na kutumika kwa uangalifu ili kiendelee kuwahudumia wananchi kwa muda mrefu.

Sumry amesema upatikanaji wa kisima hicho ni hatua muhimu katika kupunguza changamoto ya maji katika eneo hilo, akibainisha kuwa mradi huo una umuhimu mkubwa zaidi kwa wanawake ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakibeba sehemu kubwa ya jukumu la kutafuta maji kwa ajili ya familia zao.

Ameipongeza familia ya Al-Marhum Haji Abdulrahman Nkuhi kwa moyo wa kujitolea na uamuzi wa kuwekeza katika huduma yenye manufaa ya moja kwa moja kwa jamii.

Kwa mujibu wa Sumry, hatua hiyo ni mfano mzuri wa namna jamii, wadau na viongozi wanavyoweza kushirikiana katika kutafuta na kutekeleza suluhisho la changamoto zinazowakabili wananchi.

Wananchi wa Kijiji cha Manga wameeleza kufurahishwa na ujio wa mradi huo, huku wakitoa shukrani kwa familia ya Nkuhi kwa mchango huo ambao wameueleza kuwa ni wenye thamani kubwa kwa jamii yao.

Aidha, wameishukuru Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini kwa juhudi za kutafuta wafadhili na kuunga mkono upatikanaji wa huduma muhimu kwa wananchi.

Wamesema kabla ya kukamilika kwa kisima hicho walilazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji, hali iliyowafanya baadhi yao kuchangia vyanzo vya maji na wanyama katika mabwawa.

Kwa mujibu wa wananchi hao, hali hiyo ilikuwa ikihatarisha afya zao, kwani matumizi ya maji yasiyo salama yaliwafanya kukumbwa na magonjwa ya tumbo mara kwa mara.

“Tumepata faraja kubwa kwa kupata kisima hiki. Hapo awali tulikuwa tunatembea umbali mrefu kutafuta maji na wakati mwingine tunalazimika kutumia maji pamoja na wanyama. Sasa tuna matumaini ya kuishi maisha bora zaidi,” wameeleza wananchi.

Pamoja na kupata huduma ya maji, wananchi hao wameiomba Serikali kushughulikia changamoto ya ukosefu wa umeme katika kijiji hicho, wakisema kutokuwepo kwa huduma hiyo kunawakosesha fursa mbalimbali za kiuchumi.

Wamesema upatikanaji wa umeme utasaidia kuchochea shughuli za uzalishaji, biashara na uanzishaji wa miradi midogo ya kiuchumi, hivyo kuongeza kipato cha wananchi na kuchangia maendeleo ya Kitongoji cha Kaza Roho na Kijiji cha Manga kwa ujumla.

Kwa sasa, wananchi hao wameeleza kuwa wanaupokea mradi wa kisima hicho kwa matumaini makubwa, wakiamini kuwa utaondoa sehemu kubwa ya adha waliyokuwa wakiipata kwa miongo kadhaa katika kutafuta maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na shughuli nyingine za kila siku.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.