Skip to main content

KATAVI YATENGA MAENEO MAALUMU YA HUDUMA KWA WAHISIWA WA EBOLA

Na Daniel Gahu - Katavi.

KATAVI YATENGA MAENEO MAALUMU YA HUDUMA KWA WAHISIWA WA EBOLA

Na Daniel Gahu - Katavi.

Kufuatia hofu ya kusambaza kwa virusi vya Ebola, Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu pamoja na CIHEB Tanzania chini ya Mradi wa Usalama wa Afya Duniani (Global Health Security Program), imeendelea kuimarisha utayari wa kukabiliana na milipuko ya magonjwa hatari ya kuambukiza ikiwemo Ebola kupitia mafunzo ya mezani (Tabletop Simulation Exercise), yaliyowakutanisha wataalamu na wadau mbalimbali wa afya mkoani Katavi.

Akifungua mafunzo hayo yaliyowakutanisha wataalamu kutoka sekta za afya, mazingira, mifugo, wanyamapori pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama, Katibu Tawala Mkoa wa Katavi Bw. Albert Msovela amesema janga la Ebola tayari limezikumba baadhi ya nchi jirani, hivyo ni wajibu wa Mkoa wa Katavi kuendelea kujiandaa kwa kuimarisha uratibu na mwitikio wa pamoja.

"Lazima tushirikiane kwa pamoja na kuona namna gani tunaweza kukabiliana na janga hili. Wenzetu tayari limekwisha kuwakumba na huwa tunafanya nao shughuli za kijamii na shughuli za kiuchumi. Sisi kama Mkoa wa Katavi tuna mwingiliano mkubwa wa shughuli hizo, huwezi kututenganisha," amesema Msovela.

Amesema mkoa umeendelea kuweka mazingira rafiki ya kukabiliana na dharura kwa kuandaa maeneo maalumu ya kuwahudumia wahisiwa wa Ebola, ili hatua za awali ziweze kuchukuliwa kwa haraka endapo kutatokea mlipuko.

Ameongeza kuwa tayari vikao vya maandalizi vimefanyika ngazi ya mkoa na elimu imetolewa kuanzia ngazi ya mkoa hadi vijijini ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu namna ya kujikinga na kuripoti viashiria vya ugonjwa huo.

"Nitoe rai kwa wataalamu wote kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili waendelee kuchukua tahadhari na kutoa taarifa pale wanapoona kuna viashiria vyovyote. Tuendelee kusimamia maeneo ambayo yanaweza kuwa vyanzo vya maambukizi," amesema RAS Msovera.

Awali, akitoa utangulizi wa mafunzo, Mratibu wa Afya Moja kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu, Bi. Valentina Sanga, amesema mafunzo hayo yanalenga kupima uwezo wa mfumo wa afya na taasisi nyingine kukabiliana na mlipuko wa Ebola kupitia majadiliano ya kitaalamu yanayozingatia hali ya kubuniwa (scenario).

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.