Na Daniel Gahu - Katavi.
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Katavi limepokea magari 26 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 2.1, hatua inayolenga kuimarisha utoaji wa huduma za umeme na kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya shirika hilo katika mkoa huo.
Makabidhiano ya magari hayo yamefanyika leo, yakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Hozza Mrindoko, ambaye amesema uwekezaji huo unaonesha dhamira ya Serikali ya kuboresha sekta ya nishati, ili wananchi wapate huduma bora na za uhakika.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano, Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka watumishi wa TANESCO kuyatunza na kuyatumia ipasavyo magari hayo ili yaweze kufanikisha shughuli za ukaguzi wa miundombinu, matengenezo ya hitilafu za umeme pamoja na kuwafikia wananchi kwa haraka wanapohitaji huduma.
Amesema magari hayo yanatarajiwa kupunguza muda wa kushughulikia hitilafu mbalimbali za umeme, hasa katika maeneo ya vijijini na yale yaliyo mbali, hivyo kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma na kuridhisha wateja wa shirika hilo.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa TANESCO Mkoa wa Katavi, Bi. Florence Mwakasege, amesema ujio wa magari hayo ni sehemu ya mkakati wa shirika wa kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi na kuongeza uwezo wa kuwahudumia wananchi kwa wakati.
Hata hivyo, Bi. Mwakasege ameeleza kuwa pamoja na jitihada hizo, shirika hilo bado linakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazokwamisha utoaji wa huduma, ikiwemo baadhi ya wananchi kuchoma nguzo za umeme, kuiba nyaya za umeme na kuharibu miundombinu ya usambazaji wa nishati.

Amesema vitendo hivyo husababisha hasara kubwa kwa shirika na Serikali, huku vikichangia kukatika kwa huduma ya umeme na kuongeza gharama za matengenezo ya miundombinu.
Kutokana na hali hiyo, ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Katavi kushirikiana na TANESCO katika kulinda miundombinu ya umeme kwa kutoa taarifa kuhusu vitendo vya uharibifu na wizi ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.

Aidha, nao wananchi wamebainisha kuwa uwepo wa Magari hayo, wanaimani huduma ya umeme katika Mkoa wa Katavi itaimarika na kufanya wasahau adha ya kukatika kwa umeme mara kwa mara jambo ambalo linarudisha nyuma jitihada za kimaendeleo kwa wananchi.
Kupokelewa kwa magari hayo kunatarajiwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa shughuli za TANESCO, kuboresha huduma kwa wateja na kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika, hatua ambayo pia itachochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Mkoa wa Katavi.



Discussion
Reader comments
0 contributions