Na Daniel Gahu – Katavi.
Mikoa ya Katavi na Rukwa imeendelea kuimarisha ushirikiano katika kulinda na kusimamia rasilimali za asili na mazingira, baada ya wataalamu na wadau kutoka mikoa hiyo kukutana na kusaini Hati ya Makubaliano ya Uzalishaji na Uendeshaji wa Jukwaa la Ushirikiano katika Usimamizi wa Rasilimali za Asili na Maendeleo Endelevu.
Hati hiyo inalenga kuweka msingi wa ushirikiano wa pamoja katika usimamizi wa rasilimali za asili na mazingira katika mandhari ya Mikoa ya Katavi na Rukwa.
Kupitia jukwaa hilo, wadau kutoka sekta mbalimbali wanatarajiwa kushirikiana katika kupanga na kutekeleza mikakati itakayosaidia kuhakikisha rasilimali za asili zinalindwa, zinatunzwa na kutumika kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Akizungumza katika tukio hilo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Bw. Albert Msovela, amewataka wataalamu na wadau wote kuunganisha nguvu katika kusimamia rasilimali za asili kwa kuzingatia sheria, taratibu, kanuni na miongozo iliyowekwa.
Msovela amesema kila mdau ana wajibu wa kuhakikisha eneo lake la utekelezaji linazingatia misingi ya uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali.

Amesema usimamizi wa mazingira hauwezi kufanikiwa ikiwa utaachwa kwa taasisi au sekta moja pekee, bali unahitaji ushirikiano wa wadau wote.
Kwa mujibu wa Msovela, ushirikiano wa karibu baina ya taasisi za Serikali, wataalamu, wananchi na wadau wengine ni muhimu katika kukabiliana na changamoto zinazohatarisha mazingira na rasilimali za asili.
Msovela amesisitiza kuwa uharibifu wa mazingira ni miongoni mwa changamoto zinazochangia mabadiliko ya tabianchi, hivyo hatua madhubuti zinahitajika katika kulinda misitu, vyanzo vya maji, ardhi na rasilimali nyingine za asili.

Amesema uzingatiaji wa sheria na utekelezaji wa mipango ya uhifadhi ni muhimu katika kupunguza athari za uharibifu wa mazingira na kuhakikisha rasilimali zinaendelea kuwa na manufaa kwa jamii.
“Ni lazima tuungane kwa pamoja, kila mmoja kwa nafasi yake, kuhakikisha tunazingatia na kusimamia sheria, taratibu, kanuni na miongozo,” amesema Msovela.

Amesema utekelezaji wa wajibu huo kwa pamoja utaongeza ufanisi katika usimamizi wa rasilimali na kusaidia kujenga mazingira salama na endelevu kwa wananchi wa Katavi na Rukwa.
Kwa ujumla, kuanzishwa kwa jukwaa hilo kunatajwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha uratibu baina ya Mikoa ya Katavi na Rukwa, hususan katika kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira na matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali za asili.
Ushirikiano huo unatarajiwa kutoa fursa kwa wadau kubadilishana uzoefu, kuibua changamoto zinazovuka mipaka ya kiutawala na kuweka mikakati ya pamoja ya kuhakikisha rasilimali za asili zinalindwa huku zikitoa mchango katika maendeleo endelevu ya wananchi.
Discussion
Reader comments
0 contributions