Na Daniel Gahu – Katavi.
Mkoa wa Katavi unatarajia kuzindua Kamati za Ushauri wa Kisheria ngazi ya Mkoa na Wilaya, Septemba 8, 2026, katika Viwanja vya Azimio, Mpanda, huku wananchi wa Katavi na mikoa jirani wakipatiwa fursa ya kupata huduma za Kliniki ya Sheria bila malipo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 3, 2026, Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Albert Msovela, amesema Kliniki hiyo itaanza Septemba 7 hadi 13, 2026, katika Viwanja vya Azimio, Mpanda, kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni.

Amesema uzinduzi huo unatarajiwa kufanywa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, huku Mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na wataalamu kutoka taasisi mbalimbali za umma ndani na nje ya Mkoa wa Katavi wakishiriki kutoa huduma za ushauri wa kisheria kwa wananchi.
“Mgeni rasmi katika uzinduzi huo anatarajiwa kuwa Mhe. Hamza S. Johari, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, huku timu ya Mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na wataalamu kutoka taasisi mbalimbali za umma ndani na nje ya Mkoa wa Katavi wakishiriki katika utoaji wa huduma hizo,” amesema Msovela.
Kwa mujibu wa Msovela, Kliniki hiyo inalenga kuwawezesha wananchi kupata ushauri na elimu ya kisheria kuhusu masuala mbalimbali, pamoja na ufafanuzi wa hatua na taratibu zinazopaswa kufuatwa katika kushughulikia changamoto zao za kisheria.
Amesema huduma hiyo ni fursa muhimu kwa wananchi kujenga uelewa kuhusu haki na wajibu wao, pamoja na namna sahihi ya kufuata taratibu za kisheria katika kutatua changamoto mbalimbali.
“Natoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Katavi na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi katika uzinduzi huu na kutumia fursa ya Kliniki ya Sheria Bila Malipo kupata ushauri na elimu ya kisheria kuhusu changamoto mbalimbali zinazowakabili,” amesema Msovela.
Ameongeza kuwa, Mkoa wa Katavi umepata fursa ya kipekee ya kushirikisha Mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na wataalamu kutoka taasisi mbalimbali za umma, ndani na nje ya Mkoa, ambao watashiriki katika kutoa huduma za ushauri wa kisheria kwa wananchi.
“Mkoa wa Katavi umepata fursa ya kipekee ya kushirikisha Mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na wataalamu kutoka taasisi mbalimbali za umma ndani na nje ya Mkoa, ambao watashiriki katika kutoa huduma za ushauri wa kisheria kwa wananchi,” aliongeza Msovela.
Katibu Tawala huyo amesisitiza umuhimu kwa wananchi kutumia fursa hiyo kupata elimu na ushauri wa kisheria ili kufahamu haki, wajibu na taratibu sahihi za kisheria katika kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Kliniki hiyo inatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya kuwafikia wananchi moja kwa moja na kuwawezesha kupata huduma za ushauri wa kisheria bila gharama, sambamba na kuongeza uelewa wao kuhusu masuala ya sheria na taratibu zinazohusiana na haki zao.
Discussion
Reader comments
0 contributions