Na Daniel Gahu - Katavi.
Katika kuhakikisha uwajibikaji unaozingatia maadili na taratibu za utumishi wa Umma Halmashauri zote Mkoani Katavi zimetakiwa kuongeza uwajibikaji, kuimarisha mifumo ya udhibiti wa ndani na kuhakikisha hoja zote za ukaguzi ambazo bado hazijafungwa zinapatiwa majibu ifikapo Septemba 30, 2026.
Akizungumza wakati wa Mkutano Maalumu wa Baraza la Madiwani wa kupokea na kujadili taarifa ya majibu ya hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wilayani Mlele, Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Bw. Albert Msovela, amesema hatua hiyo itasaidia kuimarisha uwajibikaji na usimamizi wa fedha za umma.

“Ninatamani inapofika Septemba 30, 2026, hoja zote ambazo hazijafungwa ziwe zimepatiwa majibu,” amesema Msovela.
Amesisitiza kuwa wakurugenzi watendaji wa Halmashauri zote wanatakiwa kuhakikisha wanaongeza usimamizi wa matumizi ya mifumo iliyowekwa na Serikali ili kudhibiti kujirudia kwa hoja za ukaguzi, kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wakaguzi wa nje pamoja na kujibu hoja zote kwa wakati ili kuepusha sintofahamu.

Aidha, amewataka wakuu wa idara na vitengo kuongeza uwajibikaji na kuimarisha mifumo ya udhibiti wa ndani ili kuboresha usimamizi wa rasilimali za umma na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi.
Akifunga kikao hicho, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlele, Mhe. Soud Mbogo, amesema halmashauri itaendelea kushirikiana na wataalamu kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa, hususan katika ukusanyaji wa mapato.

“Tutaendelea kushirikiana na wataalamu wa halmashauri kuhakikisha tunafikia malengo tuliyojiwekea, hasa katika ukusanyaji wa mapato na kuboresha utendaji wa halmashauri,” amesema Mhe. Mbogo.
Kikao hicho kimejadili hatua mbalimbali za kujibu hoja za ukaguzi kwa lengo la kuimarisha uwazi, uwajibikaji na usimamizi bora wa fedha za Umma.


Discussion
Reader comments
0 contributions