Na Daniel Gahu - Katavi.
Kufuatia mfululizo wa matukio ya uporaji na unyang'anyi yaliyokuwa yakifanyika ndani ya ziwa Tanganyika lililopo Halmashauri ya wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi ilipo bandari ya Karema, Serikali kupitia Jeshi la Polisi imelikabidhi jeshi la Polisi mkoani Katavi Boti yenye kasi kubwa kwa ajili ya kudhibiti matukio hayo yaliyokuwa yakiwakumba wavuvi wa samaki na dagaa.
Akikabidhi boti hiyo Kamishna Msaidizi mwandamizi wa Jeshi la Polisi Moshi Sokoro, ambaye ni Kamanda wa Jeshi la wanamaji Tanzania amesema lengo la kukabidhi Boti hiyo yenye mwendo kasi ni kuweza kuwadhibiti wahalifu wote katika ziwa hilo.

"Nadhani nyote mmeshuhudia mwendo kasi wa boti hii, hivyo sidhani kama kuna wahalifu wenye boti yenye kasi kushinda hii hivyo naimani kuanzia leo matukio yote yanakwenda kudhibitiwa vikali" amesema Kamishna Sokoro.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi SACP Kaster Ngonyani ameimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan huku akisema kwa niaba ya wananchi na jeshi la Polisi mkoani Katavi amepokea boti hiyo kwani itawasaidia katika kufanya doria za majini katika maeneo yote ya bandari ya Karema, hususan kwa wezi ambao huwaibia wavuvi injini, samaki na vinginevyo hivyo kupitia boti hii imekuja kutibu changamoto hiyo.

Sambamba na hilo ameongeza kuwa wananchi wanao wajibu wa kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi hasa la majini ili kuweza kufanikisha oparesheni za kuwatokomeza wezi wote waliopo katika ziwa hilo, huku akibainisha kuwa jeshi la Polisi pasipo wananchi haliwezi kutokomeza matukio hayo hivyo wananchi yawapasa kutoa ushirikiano wa kutosha.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu amesema historia mpya imekwenda kuandikwa katika mwambao wa ziwa Tanganyika hususan katika bandari ya Karema kwa kuishuhudia boti yenye thamani ya zaidi ya Milioni mia nne ikiwasili katika ziwa Tanganyika ili kudhibiti matukio ya wizi wa samaki kwa wavuvi ambao wanafanya shughuli zao katika ziwa hilo.

"Boti hii inakuja kwenu wananchi ambao mnafanya shughuli mbalimbali za kiuchumi ndani ya ziwa Tanganyika, Boti hii imekabidhiwa hapa Bandari ya Karema lakini itawahudumia wananchi wote ambao pia sio wakazi wa Karema" amesema DC Buswelu.
Amesema kuwasili kwa boti hii ni tangazo rasmi kwa wahalifu na wanyang'anyi wote wanaotumia nguvu kwani boti hiyo iko tayari kuwakimbiza na kuwafukuza wezi wote kwa mwendo mkali na kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.

Aidha kwa upande wao wananchi na wavuvi wanaofanya shughuli zao za kujipatia kipato katika ziwa Tanganyika, wameishukuru Serikali kwa kuwaletea boti hiyo ya ulinzi kwasababu matukio ya unyang'anyi yamekithiri hivyo kutoka na uwepo wa boti hiyo itawasaidia sana katika maswala yakiulinzi.
"Sisi kama wavuvi tunaahidi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa shida ya aina yoyote ile ambayo tutakuwa tunaitilia shaka ndani ya maji, tutatoa ushirikiano mkubwa sana," amesema Kapezi Yahaya Seleman mwananchi na mvuvi wa samaki katika ziwa Tanganyika.

Naye Afisa mtendaji Kata Karema, Edger Richard Linda ameishukuru Serikali kwa kuwapatia boti hiyo kwani lilikuwa ni hitaji kubwa sana katika ziwa hilo ambalo limekithiri matukio mengi ya kiharifu.
"Kama wananchi itatunufaisha sana hasa kwa sisi viongozi itatusaidia katika kufanya doria pamoja na kuyafikia maeneo ya mbali ambayo tulikuwa hatuwezi kufika kuwaangalia wananchi wetu hasa wakati wanapopata ajali za majini" amesema Afisa mtendaji.
Discussion
Reader comments
0 contributions