Na Clavery Christian, Bukoba - Kagera.
Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kagera imeeleza kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, ikisema miradi hiyo inaonyesha matumizi sahihi ya rasilimali za umma na inalenga kuboresha huduma kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo wilayani humo, Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Kagera, Alhaji Nazir Mustapha Karamagi, aliipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba kwa kutumia mapato ya ndani kutekeleza miradi ya kimkakati yenye tija kwa jamii.

Miongoni mwa miradi iliyokaguliwa ni ghala la kisasa la kukausha na kuhifadhi dagaa katika mwalo wa Igabiro pamoja na Shule ya Msingi Kamagoba.
Alhaji Karamagi alisema uamuzi wa kutenga fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa ghala la Igabiro unaonyesha dhamira ya serikali ya kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi, kuboresha mazingira ya biashara na kuinua kipato cha wananchi wanaojihusisha na sekta hiyo.

Aidha, aliisifu Shule ya Msingi Kamagoba kwa ubora wa miundombinu yake, akieleza kuwa uwekezaji huo utasaidia kupunguza umbali unaotembelewa na wanafunzi kufuata elimu, kuongeza mahudhurio darasani na hatimaye kuboresha kiwango cha ufaulu.
"Niwapongeze viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba kwa kuendelea kutumia vizuri mapato ya ndani kutekeleza miradi yenye manufaa makubwa kwa wananchi. Hii ni ishara ya usimamizi mzuri wa rasilimali za umma," alisema Alhaji Karamagi.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Bi. Fatma Laay alisema halmashauri hiyo imeendelea kuwekeza mapato yake ya ndani katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayolenga kuboresha huduma za kijamii na kukuza uchumi wa wananchi.
Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa ofisi mpya za kata, ujenzi wa soko la ndizi la Kemondo, ujenzi wa maduka ya kisasa (Shopping Centre) katika eneo la Shablidini, pamoja na utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili kuwawezesha kiuchumi.

Hatua hiyo inaendelea kuifanya Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba kuwa miongoni mwa halmashauri zinazotumia mapato ya ndani kutekeleza miradi ya maendeleo yenye matokeo chanya kwa wananchi.

Discussion
Reader comments
0 contributions