Na Saulo Stephen - Singida.
Mkaguzi Mkuu wa Ndani, Boaz Kajigili amewasilisha hoja za ukaguzi zilizoibua mjadala mzito katika kikao cha Menejimenti ya Sekretarieti ya Mkoa wa Singida kilichoongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa huo, Dkt. Fatuma Mganga.
Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi mdogo wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, kililenga kuchambua na kujadili mapungufu yaliyobainishwa katika mifumo ya udhibiti wa ndani, matumizi ya rasilimali pamoja na ufuataji wa taratibu na sheria.

Kupitia hoja hizo, viongozi na watumishi walipata fursa ya kuelewa hatari zinazoweza kujitokeza endapo kasoro hizo hazitashughulikiwa kwa wakati.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Kajigili alisisitiza umuhimu wa taasisi kuchukua hatua za haraka kurekebisha dosari zilizobainishwa, ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza ikiwemo upotevu wa fedha na kushuka kwa ufanisi wa kazi.

Kwa upande wake, Dkt. Mganga alielekeza watumishi kuhakikisha wanazifanyia kazi hoja zote za ukaguzi kwa wakati, akibainisha kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza uwajibikaji, uwazi pamoja na kuimarisha nidhamu ya kazi ndani ya taasisi.
Aidha, kikao hicho kimeelezwa kuwa chachu ya kuboresha utendaji kwa kuhakikisha mapendekezo ya ukaguzi yanatekelezwa ipasavyo, jambo litakaloongeza uaminifu kwa wadau na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Discussion
Reader comments
0 contributions