Na Clavery Christian, Missenyi – Kagera.
Mradi wa ujenzi wa Soko Kuu la Kisasa Bunazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi, mkoani Kagera, umefikia asilimia 82 ya utekelezaji ndani ya miezi 11 tangu kuanza kwake, hatua inayotajwa kuwa ishara ya mafanikio katika jitihada za Serikali za kuboresha miundombinu ya biashara na kukuza uchumi wa wananchi.
Taarifa hiyo imetolewa wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kagera, iliyotembelea na kukagua maendeleo ya mradi huo wa kimkakati unaotarajiwa kuwa kitovu kikuu cha shughuli za biashara katika Wilaya ya Missenyi.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Mkoa wa Kagera, Mary Marco, alisema soko hilo linajengwa kwa mfumo wa ghorofa mbili na litakuwa na jumla ya vyumba 152 vya biashara, vyoo 28 vya kisasa pamoja na ukumbi wa mikutano utakaotumika kwa shughuli mbalimbali za kijamii na kibiashara.
Alisema ujenzi unaendelea kwa kasi na kwa kuzingatia viwango vya ubora vilivyowekwa, huku ukitarajiwa kukamilika mwezi Januari mwaka 2027.

"Mradi umefikia asilimia 82 ya utekelezaji ndani ya miezi 11 tangu kuanza kwake. Kazi zinaendelea vizuri na tunatarajia kuukamilisha kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika na huduma zitakazotolewa kupitia soko hili," alisema Mary Marco.
Aliongeza kuwa soko hilo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuboresha mazingira ya kufanyia biashara kwa kujenga miundombinu ya kisasa, salama na rafiki kwa wafanyabiashara, hatua itakayochochea biashara rasmi, kuongeza mapato ya Halmashauri pamoja na kuinua uchumi wa wananchi wa Missenyi na maeneo jirani.

Naye, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kutoka Mkoa wa Kagera, Karim Amri, alisema kukamilika kwa soko hilo kutakuwa na mchango mkubwa katika kukuza biashara, kuvutia wawekezaji na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi, hususan vijana na wanawake.
"Likikamilika, soko hili litakuwa miongoni mwa miundombinu muhimu ya biashara katika Mkoa wa Kagera. Litaboresha mazingira ya wafanyabiashara, kuongeza mapato ya ndani na kuifanya Missenyi kuwa kitovu cha biashara katika ukanda huu wa mpakani," alisema Karim Amri.

Wananchi wa Wilaya ya Missenyi wanatarajia kunufaika na mradi huo kupitia upatikanaji wa maeneo bora ya kufanyia biashara, kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi na kuboreka kwa huduma za masoko, hali itakayochangia kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na maendeleo ya wilaya kwa ujumla.
Discussion
Reader comments
0 contributions