Na Saada Almasi, Bariadi - Simiyu.
Katika kuendelea kuboresha mahusiano mazuri kwa jamii ,Jeshi la polisi mkoani Simiyu limetoa huduma za upimaji wa afya uliokwenda sambamba na utoaji elimu juu ya ukatili wa kijinsia katika kanisa na la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) mjini Bariadi mkoani humo ili waweze kutambua afya zao ambazo ni msingi muhimu wa maisha
Zoezi hilo limeongozwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi mkoani Simiyu (ACP) Edith Swebe kupitia kikosi cha afya cha Jeshi la Polisi ambapo upimaji wa Homa ya Ini na Magonjwa yasiyoambukiza kama shinikizo la damu na kisukari yakiwa miongoni wa mwa magonjwa yaliyofikiwa.

Akizungumza na Jambo Fm viwanjani hapo Kamanda Swebe amesema kuwa watu wengi wanakosa muda wa kwenda kupima afya zao mara kwa mara kutokana na hali ya utafutaji jambo ambalo linasababisha kujigundua wana matatizo kipindi ambacho ugonjwa umeshakuwa mkubwa
“muda wa kufanya uchunguzi wa afya zetu mara kwa mara umekuwa mdogo miongoni mwetu mara nyingi tupo katika shughuli za utafutaji hadi pale tatizo linapojitokeza ndiyo mtu unashtuka kuwa ugonjwa fulani ulikuwa unaishi nao,ndiyo maana sisi jeshi la polisi tumeona ni vema kuja na timu yetu hapa sehemu ya kuabudu ili kukutana na watu wengi na kuendesha huduma hii”ACP Swebe

“Pamoja na huduma za afya hapa tumekuja na dawati la jinsia ili kuweza kutoa elimu juu ya ukatili maana vipo vitendo vingi vinafanyika katika jamii ambavyo vinaathiri lakini watu hawajui wapi kwa kuripoti ama kukemea na wakati mwingine hata uoga wa kusema,sasa tunawaelimisha kwanza wavitambue vitendo hivyo lakini pia wavifichue ili kujiokoa wao jamii na jamii kwa ujumla,” ameongeza ACP Swebe.

Katika zoezi hilo pia elimu juu ya usalama barabarani imetolewa ikiwa ni pamoja na ukaguzi wa vyombo vya moto zoezi ambalo litakuwa endelevu kwa mkoa mzima ili kujenga mahusiano yenye afya baina ya Jeshi la Polisi na wananchi
Discussion
Reader comments
0 contributions