Jeshi la Polisi Wilaya ya Kasulu Mkoa wa Kigoma, limetoa msaada wa vitu mbalimbali kwa wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Mlimani iliyopo Halmashauri ya Mji Kasulu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano na kuendeleza uhusiano mwema kati ya Jeshi la Polisi na jamii.
Msaada huo uliojumuisha sabuni, mafuta ya kujipaka, kanga na nguo ulikabidhiwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Kigoma, Alfred Kasolo.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, ACP Kasolo alisema Jeshi la Polisi ni sehemu ya jamii na lina wajibu wa kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwemo kuwafariji na kuwasaidia wananchi wanaokabiliwa na changamoto za kiafya.
"Jeshi la Polisi linaendelea kutambua mchango mkubwa wa wananchi katika ushirikiano wa kudumisha amani na usalama. Kwa kutambua hilo, tumeona ni muhimu kurejesha shukrani kwa kuwafariji wagonjwa waliolazwa hospitalini na kuwapatia mahitaji muhimu," alisema ACP Kasolo.

Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mlimani ambaye pia ni Muuguzi Mfawidhi wa hospitali hiyo, Editha Yohana Vubuka, amesema msaada huo utasaidia kupunguza baadhi ya changamoto zinazowakabili wagonjwa pamoja na hospitali kwa ujumla.
Aidha amelishukuru Jeshi la Polisi kwa moyo wa upendo na huruma lilioonyesha kwa wagonjwa, akibainisha kuwa hatua hiyo ni kielelezo cha mshikamano na ushirikiano mzuri kati ya taasisi za umma na wananchi.

Baadhi ya wagonjwa waliopokea msaada huo walieleza kufurahishwa na kitendo cha Jeshi la Polisi kuwafikia hospitalini na kuwapatia zawadi hizo. Walisema hatua hiyo imewapa faraja na kuonyesha kuwa Jeshi la Polisi linajali ustawi wa wananchi si tu katika kuhakikisha usalama wao, bali pia katika nyakati wanapokabiliwa na changamoto za kiafya.
Ziara hiyo ni sehemu ya shughuli za kijamii zinazotekelezwa na Jeshi la Polisi kwa lengo la kuimarisha uhusiano na wananchi na kuendelea kujenga imani kati ya jeshi hilo na jamii.


Discussion
Reader comments
0 contributions