Na Saulo Stephen - Singida.
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Elphasi Lwanji, amesema kuwa afya ya wananchi ndiyo msingi wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi, kwani jamii yenye afya ndiyo yenye uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na kujiletea maendeleo endelevu.
Akizungumza wakati wa zoezi la tathmini ya kisiasa na kiuchumi linaloendelea ndani ya chama, Bw. Lwanji alisema maendeleo hayawezi kupatikana bila kuwa na wananchi wenye afya njema, elimu bora na mazingira yanayowezesha uzalishaji.

Alieleza kuwa CCM imeendelea kufanya tathmini ya utekelezaji wa shughuli za kisiasa na maendeleo kwa lengo la kupima mafanikio yaliyopatikana, kubaini changamoto na kuweka mikakati ya kuboresha utendaji katika ngazi zote za uongozi.
Kwa mujibu wa Lwanji, tathmini hiyo inaendelea kufanyika kuanzia ngazi ya mitaa na vijiji, kata, wilaya hadi mkoa, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya tathmini ya jumla ya utekelezaji wa shughuli za chama katika kipindi cha miaka 50. Alisema utaratibu huo unalenga kuimarisha uwajibikaji, ushirikishwaji wa viongozi na wanachama pamoja na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya chama.
Discussion
Reader comments
0 contributions