Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
Kampuni ya Jambo Group yenye makao yake makuu katika eneo la Ibadakuli, mkoani Shinyanga,inararajiwa kushiriki katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kuendelea kutangaza bidhaa zake, huduma na fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wananchi wa Tanzania na nje ya nchi.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusina na wafanyabiashara pamoja na makambuni yanayotajiwa kushiriki maonyesho hayo ya 50 ambapo amesema kampuni ya jmabo itakwenda kutangaza bidhaa zitokanazo a uongezaji wa thamni mazao ya mifugo ambapo kwa sasa kampuni hiyo imekuwa ikizalisha ikisindika maziwa na kuyahifadhi ili yaweze kudumu kwa muda murefu pamoja na bidhaa nyingine.

Amesema mbali na maziwa ,Katika maonesho hayo ya kihistoria ya miaka 50 ya Sabasaba, Jambo Group inatarajia kuonesha bidhaa zake mbalimbali zikiwemo vinywaji baridi, juisi, maji ya kunywa, biskuti, asali, mikate, pipi na aiskrimu ambazo zimekuwa zikipata soko kubwa nchini Tanzania. Ushiriki huo unalenga pia kuwapa wananchi nafasi ya kujifunza kuhusu uwekezaji, ubunifu na mchango wa kampuni hiyo katika kukuza uchumi wa taifa.
Aidha amesema Jambo Group imejijengea sifa ya kuwa miongoni mwa makampuni yanayotoa ajira kwa wananchi wengi pamoja na kuendesha shughuli zake kwa kuzingatia ubora, uwajibikaji na ubunifu. Kampuni hiyo imeendelea kuwekeza katika teknolojia za kisasa ili kuhakikisha bidhaa zake zinakidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.
Wananchi wanaotembelea Maonesho ya 50 ya Sabasaba wanahimizwa kutembelea banda la Jambo Group ili kujionea bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na kampuni hiyo, kupata elimu kuhusu huduma zake na kujifunza fursa zilizopo katika sekta mbalimbali ambazo kampuni hiyo inazihudumia.

Jambo Group ni moja ya makampuni makubwa yanayokua kwa kasi nchini Tanzania, likijihusisha na sekta mbalimbali ikiwemo uzalishaji wa vyakula na vinywaji, usafirishaji, mafuta, vifungashio na vyombo vya habari. Kampuni hiyo ilianzishwa mwaka 1998 na imeendelea kupanua shughuli zake ndani na nje ya Mkoa wa Shinyanga.
Katika hatua nyingine RC Mhita amesema mbali na wafanyabiashara na makampuni mkoa huo unatarajia kuambatana baadhi ya na vikundi vya wajasiriamali wadogo mkoani Shinyanga vinavyojishughulisha na usindikaji wa mazao nakuongeza mnyororo wa thamani ili kuvitafutia masoko viweze kuinuka kiuchumi
Maonyesho ya Biashara ya Sabasaba ni tukio muhimu linalofanyika kila mwaka nchini Tanzania kupitia Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE). Maonyesho haya hufanyika mwezi Julai katika Uwanja wa Maonesho wa Mwalimu Julius Nyerere na huwakutanisha wafanyabiashara, wazalishaji, wawekezaji pamoja na wananchi kwa lengo la kuonesha bidhaa, huduma na teknolojia mbalimbali.
Discussion
Reader comments
0 contributions