Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida, Thomas Apson amesema Halmashauri itaendelea kuongeza kasi katika ukusanyaji wa mapato ili kuwezesha kuongeza wigo wa utoaji wa mikopo ya asilimia 10.
Ameyasema hayo wakati akizindua maadhimisho ya mwezi wa Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, yaliyofanyika katika viwanja vya Ofisi ya Kijiji cha Mnang’ana, Kata ya Sepuka Mkoani humo.
Amesema ongezeko la mapato ya Halmashauri ni muhimu katika kuimarisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo na kuhakikisha wananchi wanapata fursa zaidi za kiuchumi na kusisitiza dhamira ya Serikali ya kuona wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalumu wanapata fursa ya mikopo hiyo na kuitumia kama nyenzo ya kujiimarisha kiuchumi na kuongeza kipato cha familia.
Sambamba na hilo, Apson amewataka watendaji wa Serikali katika maeneo yao kuendelea kusikiliza na kutatua kero za wananchi kwa wakati, akisisitiza kuwa utatuzi wa changamoto za wananchi ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa majukumu ya Serikali.
Amesema watendaji wanapaswa kuwa karibu na wananchi na kufuatilia changamoto zinazowakabili, akitoa mfano wa utaratibu wake wa kutenga siku ya Alhamisi kila wiki kwa ajili ya kusikiliza na kushughulikia kero za wananchi.
“Niwahakikishie kuwa Serikali iko pamoja na ninyi katika kuhakikisha maendeleo yanapatikana kwa mmoja mmoja, lakini pia kwa jamii nzima. Kila mmoja anapaswa kutekeleza wajibu wake ili tuweze kufikia maendeleo tunayoyataka,” amesema Apson.
Katika hatua nyingine amewataka wananchi kuchukua tahadhari mapema dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza kutokana na uwepo wa mvua za El Niño, kwa kuzingatia taarifa na maelekezo yanayotolewa na mamlaka husika, ikiwemo Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
Discussion
Reader comments
0 contributions