Wananchi wa Manispaa ya Tabora wameanza kunufaika na huduma za matibabu ya macho zinazotolewa bure kupitia ushirikiano kati ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora na Taasisi ya Mo Dewji Foundation.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Daktari Joseph Robert Mashafi kwa niaba ya Mo Dewji Foundation amesema kuwa mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa ambapo zaidi ya watu 680 walikuwa tayari wamejisajili kupata huduma hizo za uchunguzi na matibabu ya macho.

Amesema mpango huo unalenga kuwafikia zaidi ya wananchi 1,000 kila siku katika kipindi chote cha siku tatu za utekelezaji wake.
Dkt. Mashafi ametoa wito kwa wakazi wa Manispaa ya Tabora kuendelea kujitokeza kwa wingi ili kunufaika na huduma hizo zinazotolewa bila malipo, kwa lengo la kubaini na kutibu matatizo mbalimbali ya macho mapema.

Baadhi ya wananchi waliopata huduma hizo wameeleza kufurahishwa na hatua hiyo, wakisema imewasaidia kupata matibabu ambayo kwa kawaida yangewagharimu fedha nyingi.
Zoezi hilo linaendelea kufanyika katika Hospitali ya Wilaya ya Tabora kwa muda wa siku tatu, ambapo katika siku ya kwanza pekee zaidi ya wananchi 480 walipatiwa huduma za matibabu ya macho.

Discussion
Reader comments
0 contributions