Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora Kitete imeingia katika makubaliano na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya kuanzisha na kuimarisha huduma za magonjwa ya moyo katika Hospitali ya Kitete, hatua inayolenga kusogeza huduma hizo karibu zaidi na wananchi wa Mkoa wa Tabora na maeneo jirani.
Katika hatua za awali za utekelezaji wa makubaliano hayo, timu maalumu kutoka Hospitali ya Kitete, ikiongozwa na Mganga Mfawidhi, Dkt. Joachim Eyembe, imetembelea JKCI kwa ajili ya kujadili na kuweka mikakati ya namna ya kuanza utekelezaji wa huduma hizo katika Hospitali ya Kitete.
Ushirikiano huo unatarajiwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha uwezo wa Hospitali ya Kitete kutoa huduma kwa wagonjwa wenye magonjwa ya moyo, hususan katika uchunguzi, utambuzi wa mapema, matibabu na ufuatiliaji wa wagonjwa, hivyo kupunguza ulazima wa wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo katika hospitali nyingine.
Akizungumzia umuhimu wa hatua hiyo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Kitete, Dkt. Joachim Eyembe, amesema ushirikiano huo una umuhimu mkubwa kwa wananchi wa Tabora kwa kuwa utasaidia kusogeza huduma za moyo karibu na wananchi, kupunguza gharama za usafiri na gharama nyingine zinazoweza kujitokeza wakati wa kufuata huduma nje ya mkoa.
“Ushirikiano huu ni hatua muhimu katika kuhakikisha wananchi wa Tabora na maeneo ya jirani wanapata huduma za magonjwa ya moyo kwa wakati na karibu na maeneo yao. Tunatarajia utaongeza uwezo wa Kitete katika uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo, huku ukiwasaidia wananchi kupunguza gharama na changamoto za kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizi,” amesema Dkt. Eyembe.
Aidha, Dkt. Eyembe amesema kuimarishwa kwa huduma hizo kutasaidia kubaini magonjwa ya moyo mapema, jambo litakalowezesha wagonjwa kupata ushauri na matibabu kwa wakati na hivyo kusaidia kupunguza madhara makubwa yanayoweza kuzuilika endapo ugonjwa utagundulika mapema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge, amepongeza hatua hiyo ya ushirikiano kati ya taasisi hizo mbili, akieleza kuwa ni sehemu ya juhudi za kuendelea kusogeza huduma za kibingwa za magonjwa ya moyo karibu na wananchi.
Ushirikiano kati ya Kitete na JKCI unaweka msingi wa kuendelea kujenga uwezo wa Hospitali ya Kitete katika kutoa huduma bora za magonjwa ya moyo, sambamba na dhamira ya hospitali ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ubora na kwa wakati.
Discussion
Reader comments
0 contributions