Na Gideon Gregory - Dodoma.
Wakati vijana wengi wakihitimu vyuoni wakiwa na hofu ya ajira baadhi ya wanafunzi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) wameanza kubadili mtazamo huo wakigeuza maarifa ya darasani kuwa ubunifu, biashara na hata ajira kwa wengine.
Hatua hiyo imebainishwa leo Septemba 07,2026 Jijini Dodoma na Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA Prof. William Pallangyo wakati akizungumza na vyombo vya habari kuhusu utekelezaji wa Taasisi hiyo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa 2026/27.

"Kupitia kitengo cha ukuzaji na uendelezaji wa wanafunzi kitaaluma na kitaalamu, zaidi ya wanafunzi 5,000 wamefikiwa kupitia warsha zinazohusu ujasiriamali, ubunifu, ajira na fursa za kimataifa na zaidi ya wanafunzi 500 wamepata mafunzo mahsusi ya ujasiriamali, huku takribani 100 wakisaidiwa kuanzisha biashara ndogo ndogo," amesema.
Amesema nyuma ya takwimu hizo kuna mifano ya wanafunzi waliogeuza mawazo yao kuwa bidhaa na mifumo na biashara mfano kupitia SmartGlove, teknolojia ya kuvunja kikwazo cha mawasiliano.

"Teknolojia hiyo inalenga kutafsiri lugha ya alama kuwa maneno yanayosikika, kwa lengo la kusaidia watu wenye changamoto za usikivu katika mawasiliano,"amesema.
Prof. Pallangyo ameongeza kuwa wazo hilo lilibuniwa na kijana Damian Msonge baada ya tukio lililomgusa baada ya kushuhudia kijana mwenye ulemavu wa kusikia akifikishwa hospitalini akiwa katika hali ya dharura, lakini akakumbana na changamoto ya kueleza hali yake kwa lugha ya alama kutokana na kutokuwepo kwa mkalimani kwa wakati huo.

Katika mwaka wa fedha 2026/2027 na miaka inayofuata, taasisi hiyi inalenga pia kuimarisha uwezo wa wahadhiri na watumishi zaidi ya 400, kuboresha maktaba na intaneti, pamoja na kuendeleza matumizi ya TEHAMA katika huduma za wanafunzi na usimamizi wa taasisi.
Kwa mtazamo huo, changamoto kubwa si tu kuongeza idadi ya wanafunzi wanaohitimu, bali kuhakikisha kila mmoja anaondoka na kitu zaidi ya cheti ujuzi wa kuajiriwa, uwezo wa kujiajiri au uwezo wa kutengeneza suluhisho linaloweza kubadili maisha ya wengine.
Discussion
Reader comments
0 contributions