Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
Katika kukuza utalii mkoa wa Shinyanga kupitia wakala wa misitu (TFS), umezindua rasimi utalii wa ikolojia ili kuvutia watalii na kuongeza pato kwa serikali kupitia utalii baada ya kukamilika kwa Kituo cha Utalii Ikolojia (Ecotourism) katika Msitu wa Hifadhi wa Lubaga, mradi unaotarajiwa kuchochea watalii wengi wa ndani na nje ya mkoa na kuchechemua uchumi wa wananchi wa mkoa huo kwa kuzalisha ajira kupitia kituo hicho.
Akizungumza katika uzinduzi huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda amewataka wananchi kukitumia kituo hicho kwani uzinduzi wa kituo hicho ni hatua muhimu katika katika kuinua uchumi wa mkoa wa Shinyanga na kwamba tukio hilo si uzinduzi wa eneo la utalii pekee, bali ni hatua ya kuonyesha namna ambavyo rasilimali za asili zinaweza kubadilishwa kuwa fursa za maendeleo ya kiuchumi, ajira, elimu na burudani kwa jamii.

Amesema kwa muda mrefu watu wengi wamekuwa wakihusisha utalii na mbuga za wanyama, milima na fukwe za bahari, lakini Msitu wa Hifadhi wa Lubaga unaonyesha kuwa hata Shinyanga ina hazina kubwa ya utalii wa mazingira inayostahili kutambulika, kuendelezwa na kutembelewa na watu kutuliza akili zao kwa kufanya utalii wa ndani.
"Mkoa wa Shinyanga unaendelea kupiga hatua katika kuendeleza utalii wa ndani kwa kutumia rasilimali zilizopo. Hii ni fursa muhimu kwa wananchi wetu kujifunza kuwa utalii haupo mbali; unaweza kuanzia hapa hapa nyumbani kwetu," amesema Nkinda.

Nkinda amewataka wananchi, shule, vyuo, taasisi, makampuni na familia kutumia Msitu wa Lubaga kwa shughuli za elimu, mapumziko na burudani, akisisitiza kuwa maeneo ya asili yanasaidia pia kupunguza msongo wa mawazo na kujenga afya ya mwili na akili.
Aidha, amewahimiza vijana kutumia fursa zinazotokana na utalii wa mazingira kujiajiri kupitia huduma za wageni, biashara ndogo ndogo, ufugaji wa nyuki na shughuli nyingine zinazohusiana na uhifadhi wa mazingira.

Akisoma risala katika hafla ya uzinduzi wa msitu huo, Mhifadhi Mwandamizi wa Misitu TFS Wilaya ya Shinyanga, Fabian Balele, amesema kituo hicho kimejengwa kwa kuzingatia misingi ya uhifadhi, ambapo hakuna mti uliokatwa wakati wa utekelezaji wa mradi huo, kwani miundombinu yote imewekwa katika maeneo yasiyoharibu mfumo wa ikolojia wa msitu.
Balele amesema kituo hicho tayari kinatoa huduma mbalimbali za utalii ikiwemo utalii wa baiskeli, matembezi ya misituni, maeneo maalumu ya kupiga picha, ukumbi wa mikutano, maeneo ya kupiga kambi (Camping Sites), maeneo ya picnic pamoja na eneo maalumu la wapendao yaani Special Moments Corner kwa shughuli za kuvishana pete za uchumba na matukio mengine ya kijamii.

Ameongeza kuwa ndani ya msitu huo pia kuna shughuli za ufugaji wa nyuki zinazowezesha wageni kujifunza kuhusu Utalii wa Nyuki (Apitourism), sambamba na elimu ya uhifadhi wa mazingira, utunzaji wa miti na mimea tiba.
Amesema TFS inaendelea na mipango ya kupanua kituo hicho kwa kujenga mabwawa ya kuogelea (Swimming Pools), bustani ya wanyama, viwanja vya michezo kama mpira wa kikapu, mpira wa pete na mpira wa wavu, ukumbi mkubwa wa shughuli mbalimbali, eneo la mazoezi (Gym) pamoja na michezo ya watoto ili kukifanya Lubaga kuwa kitovu cha utalii wa mazingira katika Kanda ya Ziwa.

Mwakilishi wa Kamanda wa TFS Kanda ya Magharibi, Aloyce Kilemwa amefafanua kuwa mradi huo unalenga kuongeza thamani ya misitu ya hifadhi kupitia utalii wa mazingira unaotekelezwa kwa njia endelevu, huku ukihakikisha uhifadhi wa mazingira unaendelea kupewa kipaumbele na kwamba kupitia utalii huo, jamii na Serikali zitanufaika kiuchumi sambamba na kulindwa kwa mfumo wa ikolojia wa Msitu wa Lubaga kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Nao baadhi ya wananci waliojitokeza katika hafla ya uzinduzi wa kituo hicho wameipongeza wakala wa misitu TFS kwa hatua hiyo na kuanisha kuwa sasa mkoa wa Shinyanga utakwenda kuchangamka na kuinuka kiuchumi kupitia watalii watakaowasili katika kituo hicho kwa ajili ya utalii wa ikolojia na mambo ya asili.



Discussion
Reader comments
0 contributions