Na Saada Almasi, Maswa - Simiyu.
Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa mazingira wilayani Maswa mkoani Simiyu (MAUWASA), imemkamata na kumfikisha katika vyombo vya sheria, Haruna Mahmood mkazi wa mtaa wa Unyanyembe mjini Maswa mkoani humo, kwa kosa la kuchepusha maji kabla ya kufika kwenye mita kwa muda wa miezi mitatu mfululizo hali ambayo imeikosesha mamlaka hiyo mapato.
Mahmood amekamatwa katika ukaguzi uliofanyika katika mtaa huo na kumkuta mteja huyo akifanya biashara nyumbani kwake ya kuwauzia maji kwa wakazi wa mtaa huo bila maji hayo kusomwa katika mita.
Mhandisi kutoka mamlaka hiyo Abdulkarim Marik amesema kuwa mamlaka hiyo imebaini ubadhilifu huo baada ya kufika nyumbani kwake na kukuta huduma ya maji ikiendelea bila kupita katika mita huku majirani wa mteja huyo wakiuziwa huduma hiyo.

“Kitendo alichofanya mteja huyu ni kunyume na taratibu kwani maji hayakuwa yakifika kwenye mita hivyo alikuwa akidhulumu watumiaji wengine ambao wanategemea mapato ya mamlaka ili kuwafikishia maji maeneo yao na kujinufaisha yeye binafsi, kutokana na kitendo hicho mamlaka imemkamata na kumfikisha katika vyombo vya sheria sambamba na kukatisha huduma hiyo mahala hapo hadi pale taratibu zitakapo fuatwa,” amesema Mhandisi Abdulkarim.
Abdulkarim ameongeza kwa kutoa onyo kwa wateja wa huduma hiyo kuhakikisha wanafuata utaratibu wa matumizi ya maji hayo kwa kusema kuwa mtu ambaye atakamatwa atakabiliwa na adhabu ya faini na kifungo.
“kwa yeyote ambaye atapatikana na hatia ya kuunganisha maji na kitendo chochote kinyume na taratibu tutamfikisha katika vyombo vya sharia na adhabu yake ni kuanzia faini ya shilingi laki 5 hadi milioni 50 kulingana na ukuba wa kosa adhabu ambayo inaweza kuambatana na kifungo kwa mijibu wa sheria,” ameongeza.

Kufuatia suala hilo Jambo Fm imezungumza na Husna Mashurubu mkazi wa Bariadi ambaye ameshauri mamlaka za makoa huo kuhakikisha wanafanya ukaguzi wa mara kwa mara kwani wapo baadhi ya watumiaji hawatunzi mabomba yao na kuturirisha maji.
“huyo wamemkamata Maswa ila hata huku Bariadi wapo wengi ambao mabomba ya maji wanayapasua makusudi yanaanza kutiririsha maji hiyo inakuwa hasara niwaombe wafanye ukaguzi pia maeneo yetu ili wadhibiti na huo upotevu wa makusudi,” amesema Husna.
Discussion
Reader comments
0 contributions