Na Tryphone Odace – Kigoma.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, ameuagiza uongozi wa Halmashauri zote mkoani humo kutenga fedha kwa ajili ya kuimarisha utayari na uwezo wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.
Maelekezo hayo yametolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Dkt. Rashidi Chuachua, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, wakati akifungua kikao cha Kamati ya Afya ya msingi (PHC) Mkoa wa Kigoma kilichofanyika katika Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Dkt. Chuachua amesema Serikali inaendelea kuweka misingi imara ya kudhibiti magonjwa ya mlipuko, huku akiwataka wananchi kushiriki kikamilifu katika hatua za kinga kwa kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma, Hassan Rugwa, amesema wananchi wana jukumu kubwa la kushirikiana na Serikali katika kudhibiti uingiaji holela wa raia kutoka nchi jirani.

“Kwenye mapambano yoyote ushirikiano ni jambo muhimu hivyo, wananchi wana kila sababu ya kuungana na Serikali kukabiliana na wimbi la wahamiaji haramu wanaoingia mkoani bila kufuata taratibu, huku baadhi yao wakitoka maeneo ambayo yamethibitika kuwa na maambukizi ya Ebola,” alisema Rugwa.
Akitoa taarifa kuhusu hali ya utayari wa Mkoa wa Kigoma katika kukabiliana na ugonjwa huo, Msimamizi wa Kituo cha Operesheni za dharura za afya ya umma Mkoa wa Kigoma, Dkt. Albert Paschal, amesema mkoa huo kwa kushirikiana na Wizara ya afya umeendelea kuimarisha mifumo ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko kupitia hatua mbalimbali.

Amesema hatua hizo ni pamoja na kutambua vituo vya matibabu, kutoa elimu ya afya kwa wananchi, kutambua maeneo hatarishi katika mipaka na nchi jirani, pamoja na kuanzisha maabara tembezi kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Dkt. Paschal amesema hatua hizo zinalenga kuhakikisha mkoa unakuwa katika hali ya utayari wa haraka iwapo kutatokea changamoto ya ugonjwa wa mlipuko.

Kikao hicho kimehudhuriwa na wakuu wa taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi, viongozi wa madhehebu ya dini, wawakilishi wa vyama vya siasa pamoja na wadau mbalimbali wa masuala ya afya katika Mkoa wa Kigoma.
Mkutano huo umejikita katika kuimarisha ushirikiano wa wadau katika kuzuia na kudhibiti magonjwa ya mlipuko, pamoja na kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu hatua za kujikinga
Discussion
Reader comments
0 contributions