Na Saada Almasi, Bariadi - Simiyu.
Mkuu wamkoa wa Simiyu Anamringi Macha ameipongeza Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani humo kwa kuvuka lengo la makusanyo ya mapato ya ndani kwa kukusanya kiasi cha shilingi Bilioni 3 na milioni 700 sawa na asilimia 100.15 ya lengo kusudiwa.
Macha ametoa pongezi hizo katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo kilichoketi kusikiliza na kujadili hoja za mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2025/2026 na kusema kuwa mafanikio ambayo wameyapata yanatokana na uzingatiaji mzuri wa maelekezo ya serikali.

“Hiki ni kielelezo kinachoonyesha kuwa sasa mnafanya uzingatiaji kwa vitendo maelekezo ya serikali ya kuhakikisha makusanyo ya mapato ya kila halmashauri yanaongezeka .Bila haya makusanyo maendeleo kuyapata itakuwa kazi kubwa lakini ninaona jitihada zenu za kumuunga mkono Rais wetu jambo moja niwaombe endeleeni kuongeza kasi ya makusanyo lakini pia muwe na usimamizi mzuri wa mifumo ili kinachopatikana kisomane na mfumo mwingine,” amesema RC Macha.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Bariadi, Ibrahim Kijanga ameishauri halmashauri hiyo kubuni vyanzo vipya vya mapato ambavyo vinaweza kutumika kukuza uchumi kwa kuongeza mapato kwani bado sekta nyingi ambazo zinaweza kugeuzwa fursa.

“Huu mji wetu bado kuna maeneo mengi ambayo tukiyatumia ipasavyo yanaweza kuwa vyanzo vizuri vya mapato. Hapa mnasifiwa kwa mapato kuzidi makadirio lakini fursa zingine hamkuzitumia ninaamini mkibuni vyanzo vingine vingi zaidi tutapata makusanyo maradufu,” amesema Ibrahim Kijanga.
Sambamba na hilo halmashauri hiyo imeendelea kupokea hati safi kutoka ofisi ya mkaguzi wa serikali (CAG) licha ya hoja nne ambazo kwa kipindi cha mwaka wa fedha ulioisha hazikutimia na kutokana na hali hiyo Mkuu wa Mkoa huo, Anamringi Macha pamoja na Mkaguzi wa nje Fortunatus Donge wameitaka halmashauri hiyo kuhakikisha zinatimia maelekezo ambayo yamepokelewa na mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Nkenyernge Charles.

“Niahidi kwamba maelekezo yenu tumeyapokea na ni matarajio yetu kuwa tunakwenda kufanyia kazi kwatika mwaka huu mpya wa fedha,“ amesema Charles.

Discussion
Reader comments
0 contributions