Na Saulo Stephen - Singida.
Katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani, Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga, amezielekeza halmashauri zote ambazo bado hazijaanza kutumia moduli za maegesho na usajili wa majengo katika Mfumo wa TAUSI kufanya hivyo mara moja, huku akizitaka kutenga asilimia 20 ya bajeti kwa ajili ya usajili wa majengo ili kupanua wigo wa mapato na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Akifungua mafunzo ya Moduli ya TAUSI yaliyofanyika katika Chuo cha VETA Singida kwa washiriki kutoka mikoa ya Singida, Dodoma, Morogoro na Iringa, Dkt. Mganga amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato kupitia TAMISEMI.

Amesema moduli ya maegesho imeongeza mapato kutoka shilingi bilioni 20 mwaka 2022/2023 hadi bilioni 36 mwaka 2025/2026 katika halmashauri 52 pekee, akisisitiza kuwa halmashauri zilizobaki zinapaswa kutumia fursa hiyo kuongeza mapato.
Aidha, amewataka waweka hazina, wahasibu na wataalamu wa TEHAMA kuutumia mfumo wa TAUSI kwa uadilifu na kuepuka kuuhujumu, akisisitiza kuwa changamoto si mfumo bali watumiaji wake. Ameongeza kuwa usajili sahihi wa majengo utaongeza mapato ya kodi za majengo, kuboresha taarifa za makazi na kurahisisha wananchi kupata huduma mbalimbali ikiwemo mikopo ya elimu.

Mwenyekiti wa mafunzo hayo, Bw. Nicolous John Alabha, amesema kikao kazi hicho cha siku nne kinalenga kuwajengea uwezo washiriki kuhusu matumizi ya moduli za maegesho na kodi za majengo ili kuongeza mapato ya halmashauri zote 184 nchini na kupunguza utegemezi wa vyanzo vya mapato vinavyoathiriwa na mabadiliko ya hali ya hewa.
Naye Mkaguzi wa Ndani Mkuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu–TAMISEMI, Mjanja Hamis, amesema mafunzo hayo yamelenga kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya maegesho na kodi za majengo kwa kuwawezesha wahasibu, waweka hazina na maafisa TEHAMA kutumia kikamilifu moduli za TAUSI.

Discussion
Reader comments
0 contributions