Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Joseph Kabila, ametangaza kuchukua uongozi wa muungano mpya wa kisiasa na kijeshi unaojulikana kama Front for the Refoundation of the Nation (FRN), ikiwa ni mbadala wa M23 ama AFC.
Muungano huo, umetangazwa rasmi katika mji wa Goma uliopo mashariki mwa DRC, unawakutanisha viongozi wakuu kutoka kundi la waasi la AFC/M23 na kujipanga upya katika safu ya kuipinga serikali ya Kinshasa inayoongozwa na Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo.

Akitangaza kuundwa kwa muungano huo kwenye mkutano na waandishi wa habari, mshauri wa muungano huo, Claude Ibalanky, amesema lengo kuu ni kuunganisha nguvu za upinzani nchini humo DRC.
"Wajibu wa Front for the Refoundation of the Nation ni kuunganisha na kuratibu majeshi yote ya upinzani ili kukomesha utawala wa kitisho—kwa kutumia njia yoyote inayowezekana, ikiwa ni pamoja me nguvu—na kuweka mwelekeo mpya pamoja na kuunda fursa mpya kwa ajili ya nchi," alisema Ibalanky.
Aidha katika kauli yake hiyo aliongeza kuwa walioweka saini wameamua kuunganisha nguvu, rasilimali, na mbinu zao ili kuunda mfumo wa utendaji utakaowawezesha Wakongo wote kushirikiana katika jukumu la "kuikomboa nchi yao."

Kuundwa kwa FRN kunajiri katikati ya mabadiliko makubwa ya kimkakati miongoni mwa makundi yanayopinga utawala wa DRC. Katika taarifa ya mwezi Juni, Ripoti ya Wataalamu wa Umoja wa Mataifa (UN) imeashiria uwezekano wa kundi la AFC/M23 kujipanga upya, ikihusisha mabadiliko ya jina na Joseph Kabila kuchukua nafasi ya uongozi.

Akizungumza kwenye mkutano huo wa Jumatatu, mwanachama wa muungano huo, Moïse Nyarugabo, ametoa onyo la moja kwa moja kwa Rais Félix Tshisekedi akisema...
"Leo hii, ujumbe kwa Tshisekedi ni kwamba lazima afanye uchaguzi. Akitaka amani, tuko tayari kumpa; akichagua vita, pia ataipata."
Hadi sasa, serikali ya Rais Félix Tshisekedi haijatoa tamko rasmi kuhusu hatua hiyo mpya walakini Mwaka jana, mahakama nchini DRC ilimhukumu Joseph Kabila adhabu ya kifo akiwa hayupo nchini (in absentia), kwa makosa yanayojumuisha usaliti wa taifa sambamba na uhalifu wa kivita.

Hata hivyo, Rais huyo wa zamani alikanusha vikali kuwa na uhusiano wowote na kundi la M23 au serikali ya Rwanda, huku akipinga hukumu hiyo na kuitaja kuwa kesi ya kisiasa yenye lengo la kuchafua taswira yake kama Mwanasiasa mkongwe na mwenye mchango mkubwa kwa Taifa lake.
Discussion
Reader comments
0 contributions