Gumzo kubwa limeibuka baada ya Kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki Ulimwenguni, Papa Leo XIV, kufanyiwa upasuaji uliondoa uvimbe wa saratani ugonjwa uliokuwa ukidhoofisha afya yake.
Upasuaji huo umedumu kwa muda wa takribani dakika 90 uliofanikiwa kuondoa uvimbe wenye saratani katika pafu lake la kulia na kurejea katika hali ya kawaida.
kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Vatican ofisi ya kiongozi huyo, upasuaji huo uliofanyika katika Hospitali ya Gemelli mjini Roma, ukihusisha kuondolewa kwa sehemu ya chini ya pafu lake la kulia (lower lobe) ili kuondolewa kwa seli za saratani.
"Upasuaji huo umethibitisha utambuzi wa saratani ya mapafu aina ya pulmonary adenocarcinoma, kama ilivyohisiwa wakati wa vipimo vya kabla ya upasuaji. Upasuaji umefanikiwa bila matatizo yoyote," ilieleza taarifa rasmi ya Vatican.

Duru kutoka Vatican zimeeleza kuwa Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 71 aliamka vyema na hata kuomba chakula cha jioni baada ya upasuaji kumalizika. Hata hicyo Madaktari wanaendelea kufanya vipimo zaidi ili kubaini ikiwa saratani hiyo imesambaa sehemu nyingine za mwili.
Mtaalamu wa afya kutoka Chama cha Mapafu cha Marekani (American Lung Association), Dkt. Juanita Mora, ameiambia AFP kuwa saratani ya aina hii iligundulika mapema, huku kukiwapo na uwezekano wa kupona kikamilifu.
"Aina hii ya saratani inapogundulika katika hatua za awali na kufanyiwa upasuaji kabla haijasambaa, kiwango cha wagonjwa kuishi kwa miaka mitano au zaidi hufikia kati ya asilimia 80 hadi 98," alisema Dkt. Mora, akiongeza kuwa madaktari watatathmini ikiwa atahitaji matibabu ya ziada kama vile chemotherapy, mionzi, au matibabu maalum ya kinga (immunotherapy).

Papa Leo XIV ambaye alizaliwa mjini Chicago na kuwa mmarekani wa kwanza kushika wadhifa huo tarehe 8 Mei, 2025 anajulikana kwa kupenda michezo na kuwa na afya njema kwa ujumla. Hii ni mara yake ya kwanza kulazwa hospitalini tangu achaguliwe kuwa kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki.

Vatican imeeleza kuwa inatarajia kipindi cha matibabu na kupona hospitalini kitachukua takriban wiki moja. Huku Mikutano yake yote ya hadhara (audiences) ikifutwa hadi tarehe 20 Oktoba.
Hata hivyo, upasuaji huo umeibua maswali kuhusu uwezekano wa kuahirisha ziara yake ndefu ya kichungaji iliyopangwa kufanyika Amerika ya Kusini kuanzia tarehe 6 hadi 17 Novemba, ambapo alitarajiwa kutembelea nchi za Uruguay, Argentina, na Peru.
Discussion
Reader comments
0 contributions