Na Gideon Gregory - Dodoma.
Imeelezwa kuwa ugonjwa wa Tezi la shingo (Goita) ni miongoni mwa magonjwa yasiyoambukiza, ambapo wanawake wanahatari zaidi ya kupata ugonjwa huu kuliko wanaume.
Tafiti zinaonesha kuwa wagonjwa 9 kati ya 10 ni wanawake, aidha wanawake 12 kati ya 100, wanahatari ya kupata ugonjwa huo.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi leo Aprili 15, 2026 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mariam Mungula, aliyehoji Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kwa wanawake juu ya magonjwa ya Tezi ya Shingo (Thyroid disease) yanayopelekea ukomo wa hedhi (Perimenopause).

Dkt. Samizi amebainisha kuwa visababishi vya ugonjwa huo ni tezi ya shingo kushambuliwa na kinga ya mwili (autoimmune), kupanda na kushuka kwa homoni (estrogene, progestrone, Thyroid) katika mazingira ya upungufu wa madini joto mwilini, Familia (Genetics), umri zaidi ya miaka 60 na msongo wa mawazo na namna ya maisha .
"Serikali inatekeleza Mpango wa utoaji elimu kwa Wanawake juu ya Magonjwa ya Tezi ya Shingo kwa kutoa elimu kwa jamii kupitia vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo redio, runinga, mitandao ya kijamii, mabango na vipeperushi kuhusu chanzo dalili na kinga ya ugonjwa," amesema.
Ameongeza kuwa serikali inasimamia na kuhakikisha chumvi yote inayozalishwa na kuuzwa nchini inakuwa na kiwango stahiki cha madini joto.
"Serikali imeimarisha kampeni jumuishi za lishe kwa kuendelea kuhamasisha matumizi sahihi ya vyakula vyenye madini joto na lishe bora," ameongeza.
Amesema Serikali imeendelea kutoa elimu na kuhamasisha jamii kutumia vyakula vyenye madini joto ikiwemo; chumvi yenye madini joto pamoja na vyakula vyenye madini joto.
"Kuimarisha na kupanua wigo wa uchunguzi, upatikanaji wa vipimo, na huduma za matibabu ya magonjwa ya tezi katika ngazi zote za huduma za afya," amesema.
Pia, kuwajengea uwezo watoa huduma za afya ili waweze kutambua mapema na kutoa huduma sahihi kwa wagonjwa wa tezi ya shingo.
Discussion
Reader comments
0 contributions