Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) mkoa wa Geita imetakiwa kuweka nguvu na mkazo wa ushiriki wa wadau wa Sekta ya Afya kushiriki katika warsha za mapambano dhidi ya rushwa kutokana na sekta hiyo kubeba mustakabali wa uhai wa watu.
Mkuu wa wilaya ya Geita,Hashim Komba ameeleza hayo Oktoba 28,2026 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Geita wakati akifungua warsha ya mapambano dhidi ya Rushwa iliyoandaliwa na Mgodi wa dhahabu wa Geita(GGML)kwa ushirikiano na TAKUKURU Mkoa wa Geita akieleza kuwa endapo vitendo vya rushwa havitodhibitiwa katika sekta hiyo basi kundi kubwa la watanzania linaweza kupata athari.
"Wafawidhi kuanzia ngazi za zahanati,vituo vya afya,hospitali za wilaya, haya ni miongoni mwa maeneo muhimu sana na wadau muhimu sana wa kualikwa kwenye warsha kama hizi kwasababu ni sekta ambazo zimebeba mustakabali wa uhai wa watu"amesema DC Komba

Mkuu wa wilaya ya Geita,Hashim Komba akitoa hotuba kwenye warsha ya makabiliano dhidi ya rushwa iliyofanyika kwa Ushirikiano kati ya Mgodi wa dhahabu wa Geita(GGML) na TAKUKURU Geita,iliyofanyika katika Ukumbi wa Golden Social Hall,Manispaa ya Geita.
Akizungumza kuhusu malengo ya warsha hiyo,Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Geita,Alex Mpemba ameeleza kwamba elimu ya makabiliano dhidi ya rushwa pia ni muhimu katika sekta ya Madini kutokana na kuwa na mchango muhimu katika kuchangia ajira,mapato serikalini,miradi ya maendeleo na fursa za kibiashara kwa wananchi.
"Ni wazi kwamba uwepo wa GGML ndani ya mkoa wetu wa Geita,pamoja na shughuli nyingine nyingi wanazofanya,unatoa fursa nyingi zenye manufaa kwa wananchi,ili fursa hizi ziweze kuwa endelevu na kuleta manufaa makubwa ya kudumu,ni muhimu kuhakikisha kwamba shughuli za uwekezaji na maendeleo zinaendeshwa kwa uwazi na uwajibikaji,kuzingatia misingi ya sheria weledi na uadilifu mkubwa na hapo ndipo ushirikiano kati ya GGML na TAKUKURU unajitokeza"amesema Mpemba

Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Geita,Alex Mpemba akizungumzia malengo ya warsha ya mapambano dhidi ya rushwa ndani ya mkoa wa Geita.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML),Duan Campbell amesema kuzuia rushwa halipaswi kuwa jukumu la TAKUKURU pekee wala Taasisi za serikali pekee bali linapaswa kuendelea kuwa jukumu letu sote,akisistiza kuwa uaminifu unaweza kupotezwa na vitu vidogo hususani vitendo vya rushwa.
‘Sera na taratibu ni muhimu, mifumo ya udhibiti ni muhimu, na mifumo ya kuhakikisha uzingatiaji wa sheria na kanuni ni muhimu, Hii ina maana kwamba jukumu la kuzuia rushwa hawawezi kuachiwa TAKUKURU pekee, haliwezi kuachwa kwa idara zinazoshughulikia uzingatiaji wa sheria, uongozi, au taasisi za serikali pekee ni jukumu letu sote’amesema Campbell

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML),Duan Campbell akisistiza umuhimu wa makabiliano ya rushwa ndani ya mkoa wa Geita.
Mwenyekiti wa serikali ya Mtaa wa Msalala Road,Sostenes Kalisti ambaye ni miongoni mwa washiriki wa warsha hiyo amesema semina za aina hiyo zimekuwa na manufaa kwao katika mapambano dhidi ya rushwa katika shughuli zao za kila siku wanapohudumia wananchi wakati
Nae Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Lwenge,Dismas Joseph ameeleza kuwa awali walikuwa hawana elimu ya makabiliano dhidi ya rushwa na kushukuru ushirikiano wa TAKUKURU na GGML kwa kuwapatia elimu hiyo ambayo imekuwa msaada katika utekelezaji wa shughuli zao za kila siku.
Warsha hiyo ya siku moja imehusisha wadau mbalimbali kutoka katika sekta za madini,wakiwemo wakandarasi wanaofanya kazi na mgodi wa GGML,wadau kutoka sekta ya elimu,asasi za kiraia,viongozi wa dini na wanafunzi wanaounda klabu za kupinga rushes shuleni.
Discussion
Reader comments
0 contributions