Skip to main content

GGML YATUNUKIWA TUZO MBILI ZA MLIPA KODI

Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imetunukiwa Tuzo mbili za Rais za Walipakodi, ikitambuliwa kuwa mlipakodi namba moja nchini na kampuni inayozingatia kwa kiwango cha juu zaidi sheria za kodi kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

GGML YATUNUKIWA TUZO MBILI ZA MLIPA KODI

Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imetunukiwa Tuzo mbili za Rais za Walipakodi, ikitambuliwa kuwa mlipakodi namba moja nchini na kampuni inayozingatia kwa kiwango cha juu zaidi sheria za kodi kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Tuzo hizo zilitolewa katika maadhimisho ya miaka 30 ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yaliyofanyika Jumanne katika Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City, Dar es Salaam, chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Maadhimisho hayo yalibeba kaulimbiu isemayo "Miaka 30 ya TRA, Mlipakodi Shujaa, Tanzania Inajitegemea," na yaliwakutanisha viongozi wa Serikali, wafanyabiashara pamoja na wadau mbalimbali kwa lengo la kutambua walipakodi wanaotekeleza wajibu wao kwa uadilifu na hivyo kuchangia utoaji wa huduma za umma, maendeleo ya taifa na agenda ya kujitegemea.

Tuzo hizo zilipokelewa na Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Ashraf Suryaningrat, akiwa ameambatana na Makamu wa Rais wa Kampuni anayesimamia Uendelevu na Ushirikishwaji wa Wadau, Simon Shayo, pamoja na Meneja Mwandamizi wa Migogoro ya Kodi, Godvictor Lyimo.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hizo, Ashraf Suryaningrat alisema heshima hiyo ni matokeo ya juhudi za pamoja za wafanyakazi, wasambazaji na wadau wote wanaoshirikiana na kampuni.

"Utambuzi huu unaakisi kazi kubwa inayofanywa na kila mfanyakazi wa Kitanzania, kila msambazaji na kila mshirika ambaye amechangia kufanikisha viwango hivi vya utendaji. Sekta ya madini ina nafasi muhimu katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya Tanzania, na ulipaji wa kodi kwa uaminifu ni moja ya njia muhimu zaidi tunazotimiza wajibu wetu kwa taifa," alisema.

Alieleza kuwa tuzo hizo zina umuhimu mkubwa katika muktadha wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo imeitambua sekta ya madini kuwa moja ya nguzo kuu za kufanikisha azma ya Tanzania kuwa na uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050.

Kwa mujibu wa Dira hiyo, sekta ya madini inatarajiwa kuendelea kuchochea ajira, kuongeza mapato ya mauzo ya nje, kuimarisha viwanda vinavyotegemea madini pamoja na kuongeza thamani ya rasilimali za nchi. Kutambuliwa kwa GGML kama mlipakodi bora na kampuni inayozingatia sheria za kodi kunadhihirisha mchango wa uchimbaji madini unaowajibika katika kufanikisha ajenda hiyo ya kitaifa.

Tangu kuanza shughuli zake nchini, GGML imechangia zaidi ya dola za Marekani bilioni 3.7 kupitia kodi mbalimbali kwa Serikali ya Tanzania.

 Tuzo za mwaka 2026 zinaendeleza rekodi ya mafanikio ya kampuni katika uzingatiaji wa sheria za kodi. Katika mwaka wa fedha 2021/2022, GGML ilitambuliwa kama mlipakodi bora zaidi katika sekta ya madini na pia ilipokea tuzo ya mchango mkubwa kupitia mauzo ya bidhaa nje ya nchi. Mwaka wa fedha 2020/2021, kampuni hiyo ilishika nafasi ya pili kwa kuwa mlipakodi mkubwa zaidi nchini.

Mnamo mwezi Oktoba 2025, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, alitembelea rasmi shughuli za GGML mkoani Geita wakati wa Wiki ya Huduma kwa Wateja, ambapo aliitambua kampuni hiyo kuwa miongoni mwa walipakodi wakubwa na wanaozingatia sheria za kodi nchini.

Kwa sasa, Kampuni ya GGML imeajiri zaidi ya watu 7,000, ambapo asilimia 98 ni Watanzania. Kampuni hiyo pia inashirikiana na zaidi ya kampuni ndogo na za kati 600 za Kitanzania katika mnyororo wake wa ugavi na mtandao wa biashara, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera na kanuni za maudhui ya ndani (Local Content) nchini Tanzania.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.