Na Ibrahim Rojala, Mwanza.
Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML), umeshiriki kikao cha Kamati ya Usalama ya Chemba ya Madini Tanzania (TCM) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, kilicholenga kuimarisha usalama wa migodi, mahusiano na jamii zinazozunguka maeneo ya uchimbaji pamoja na ushirikiano kati ya sekta ya madini na vyombo vya dola.
Kikao hicho kilifanyika katika Hoteli ya Malaika jijini Mwanza na kuhudhuriwa na Kamishna wa Kamisheni ya Polisi Jamii, CP Alex Mkama, Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Geita, ACP Amina Kahando, pamoja na wawakilishi wa kampuni mbalimbali za madini nchini.
Mbali na GGML, kampuni zilizoshiriki ni pamoja na Shanta Mining, Buckreef Gold Mine na Barrick North Mara.
Katika kikao hicho, kila kampuni iliwasilisha uzoefu wake kuhusu usimamizi wa ulinzi na usalama, ushirikiano na jamii zinazozunguka migodi pamoja na utekelezaji wa programu za Polisi Jamii.

Akizungumza katika kikao hicho, Mratibu wa Ulinzi, Haki za Binadamu, Polisi Jamii na Misitu wa GGML, Mihinzo Tumbo, alisema utekelezaji wa programu ya Polisi Jamii umeleta mafanikio makubwa katika kuimarisha usalama wa mgodi na mahusiano na wananchi.
Alisema programu hiyo imechangia kupungua kwa asilimia 81 ya matukio ya uchimbaji haramu, kupungua kwa uvamizi wa mgodi, matumizi ya silaha, pamoja na matukio ya watoto na wanawake kuingia mgodini kinyume cha sheria.
“Mahusiano kati ya mgodi na vijiji vinavyozunguka eneo la mgodi yameimarika. Makubaliano tuliyofikia na vijiji na mitaa yamesaidia kuondoa utaratibu wa wananchi kuchangishwa fedha. Aidha, baada ya kudhibiti uvamizi, vijana wengi wamepata ajira na uharibifu wa misitu umepungua kupitia vikundi vya ulinzi shirikishi,” alisema Tumbo.
Aliongeza kuwa idadi ya watu wanaoingia mgodini kinyume cha sheria imepungua kutoka watu 9,762 mwaka 2014 hadi 1,881 mwaka 2026.
Pia alisema kupitia programu za utoaji elimu katika vijiji na mitaa inayozunguka mgodi, maeneo yaliyofikiwa yalishuhudia utulivu wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 bila kuripotiwa vurugu, vifo au majeruhi.

Hata hivyo, alibainisha kuwa bado kuna changamoto katika utekelezaji wa programu hiyo, ikiwemo baadhi ya vijana kudaiwa kuombwa rushwa ili kuidhinishiwa kujiunga na vikundi vya ulinzi shirikishi.
“Tunashirikiana na TAKUKURU kukabiliana na changamoto hii. Vilevile, baadhi ya vijana wasio waaminifu hushirikiana na wavamizi na wachimbaji haramu,” alisema.
Alisisitiza kuwa programu ya Polisi Jamii imekuwa na manufaa kwa jamii, kampuni na Mkoa wa Geita kwa ujumla, huku akiishukuru Jeshi la Polisi kwa ushirikiano wake katika kuhakikisha programu hiyo inafanikiwa.
Katibu Mkuu wa Chemba ya Wachimbaji Madini Tanzania (TCM), Mhandisi Benjamin Mchwampaka, alisema kikao hicho kimekuwa jukwaa muhimu la kujadili namna ya kuimarisha usalama, mahusiano na ushirikiano kati ya wawekezaji wa sekta ya madini, Jeshi la Polisi na jamii zinazozunguka migodi.
Alisema ushiriki wa Kamishna wa Kamisheni ya Polisi Jamii umetoa fursa kwa wadau kuwasilisha changamoto na mapendekezo ya maboresho.
“Tumekubaliana kuwa kuanzia sasa tutakuwa tunakutana mara mbili kwa mwaka, katika robo ya pili na ya nne, ili kufuatilia utekelezaji wa maazimio tuliyokubaliana,” alisema Mchwampaka.
Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Geita, ACP Amina Kahando, aliipongeza GGML kwa mchango wake katika kuimarisha uwezo wa Jeshi la Polisi kupitia utoaji wa pikipiki, ujenzi wa nyumba za askari pamoja na kuboresha vituo vya polisi, ikiwemo Kituo cha Polisi Chato.
Alisema ushirikiano huo umeimarisha utekelezaji wa programu ya Polisi Jamii kupitia utoaji wa elimu, operesheni za kuzuia uvamizi wa migodi na uanzishaji wa vikundi vya ulinzi shirikishi.
“Kupitia falsafa ya Polisi Jamii tumekuwa tukitoa elimu ya ulinzi shirikishi, kuimarisha uwezo wa askari na kuhamasisha wananchi kutoa taarifa za viashiria vya uhalifu. Ushirikiano huu umechangia kupungua kwa kiwango kikubwa kwa matukio ya uhalifu katika maeneo ya migodi,” alisema ACP Kahando.
Naye Kamishna wa Kamisheni ya Polisi Jamii, CP Alex Mkama, alisema maelekezo ya Mkuu wa Jeshi la Polisi ni kuzuia uhalifu kwa kuwekeza zaidi katika elimu, ushirikiano na jamii pamoja na matumizi ya taarifa za kiintelijensia badala ya kusubiri matukio yatokee.
Aliwataka wawekezaji kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kutekeleza mkakati huo na kutoa taarifa kwa uwazi kuhusu changamoto wanazokutana nazo ili zipatiwe ufumbuzi.
“Tunataka migodi iendeshe operesheni salama zinazozingatia haki za binadamu na zisizoleta madhara. Pia tunaomba ushirikiano katika kuwajengea uwezo askari wa Polisi Jamii kupitia mafunzo mbalimbali,” alisema CP Mkama.
Kwa upande wa wadau wengine, Meneja wa Ulinzi wa Barrick North Mara, Deusdedith Masimba, alisema kuanzia mwaka 2019 mgodi huo umeimarisha mifumo ya ulinzi kiasi kwamba matukio mengi ya uvamizi huzuiwa kabla wahusika hawajaingia mgodini.
Alisema wastani wa matukio ya uvamizi umeshuka kutoka matukio 11 kwa siku mwaka 2023, hadi matano mwaka 2024, na kufikia wastani wa tukio moja kwa siku mwaka huu, huku wakati mwingine mwezi mzima ukipita bila tukio lolote.
Aidha, alisema kati ya watu 65 waliokamatwa, 56 wamepatikana na hatia mahakamani kutokana na ushirikiano mzuri wa wananchi na vikundi vya sungusungu katika kutoa ushahidi.
Masimba aliongeza kuwa asilimia 51 ya wafanyakazi wa mgodi huo wanatoka katika vijiji 11 vinavyozunguka mgodi, huku sungusungu 596 na askari polisi 154 wakishiriki katika shughuli za ulinzi saa 24.
Naye Daniel Francis kutoka Buckreef Gold Mine alisema matumizi ya vikundi vya sungusungu yamechangia kuimarisha usalama wa mgodi huo.
Alisema mgodi umeajiri sungusungu wanane na unapanga kuongeza idadi yao katika bajeti ijayo ili kukidhi mahitaji ya kiusalama.
“Tunashirikiana na viongozi wa vijiji katika kupata vijana wenye sifa za kuajiriwa,” alisema Francis.
Discussion
Reader comments
0 contributions