Na Ibrahim Rojala, Nkome - Geita.
Baadhi ya wakazi wa Kata ya Nkome, Wilaya ya Geita, ambao kwa miaka mingi walitegemea shughuli za uvuvi katika Ziwa Victoria kama chanzo kikuu cha kipato, wameanza kuona mwanga mpya wa kiuchumi baada ya kukabiliwa na changamoto zilizokuwa zikiwalazimu kusafiri umbali mrefu kutafuta samaki bila ya kuwa na uhakika wa kuwapata.
Mabadiliko hayo yamechangiwa na utekelezaji wa mradi wa ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba unaotekelezwa na Kikundi cha Jiendeleze Mchangani, ambapo wanachama wake sasa wameanza kuvuna matunda ya uwekezaji huo.

Juni 25, 2026 imekuwa siku ya kihistoria kwa wanachama 33 wa kikundi hicho nyenye muda wa miaka mitano tangu kuanzishwa kwake baada ya kufanikisha uvunaji wao wa kwanza wa samaki waliopandikizwa katika vizimba vitano vilivyowekwa ndani ya Ziwa Victoria,Mradi unaotekelezwa kwa gharama ya kiasi cha shilingi milioni fedha ambazo ni ufadhili kutoka kwa mgodi wa dhahabu wa Geita (GGML).
Mradi huo umehusisha upandikizaji wa zaidi ya vifaranga 100,000 vya samaki, hatua iliyowezesha kufanyika kwa mavuno hayo ambayo yanatajwa kuwa mwanzo wa safari mpya ya kujikwamua kiuchumi kwa wanakikundi hao.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Jiendeleze Mchangani, Daniel Mazota amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano, uvumilivu na kujituma kwa wanachama wote wa kikundi tangu kuanzishwa kwa mradi huo hadi kufikia hatua ya mavuno.
Kwa upande wake, Afisa Mwandamizi wa Uratibu na Usimamizi wa Miradi ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kutoka Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML), Masaki Godlove, amesema mradi huo uliogharimu kiasi cha shilingi milioni 251 umeanzishwa kwa lengo la kuwajengea kujiamini watu mbalimbali kuwa inawezekana kufuga samaki kwa njia ya vizimba na fedha ikapatikana.

“Wanufaika tumewapa vitu kadhaa ambavyo unaweza kuvithaminisha kwenye fedha,tumewapa vizimba vine,tumewapa vifaranga jumla 120,000,tumewapa vyakula tani 36 lakini pia tumewapa boti,tumewapa kamera,taa za sola kwaajili ya ulinzi lakini tumewapa mtaalamu ambaye anakuwa ni wa muda wote hapa kwaajili ya kuwa coach na kuwa monitor” amesema Masaki.
Masaki ameeleza kuwa GGML inatekeleza mradi huo endelevu kwa njia ya kutenga kiasi cha fedha kutoka katika mafuno ambapo fungu la kwanza la fedha zinazotokana na mavuno zinatengwa ambapo fungu la kwanza litakuwa ni kwa lengo la kutunza mtaji,fungu la pili zikielekezwa kwenye gharama zinazorejeshwa kwenye mradi na baada ya mavuno kufanyika mara tatu matarajio ni kwamba mtaji utakuwa umerudi na kukabidhi fedha hizo kwa kikundi kingine wakati kikundi cha kwanza kikibaki na vifaa vya kuendeleza mradi.

Nae Diwani wa kata ya Nkome ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Christopher Kahesi, amesema mradi huo umeanza kuonesha mafanikio makubwa wakiutarajia kuongeza ajira, kuimarisha shughuli za uzalishaji mali na kuinua kipato cha wananchi wa eneo hilo.
“Niwashukuru sana Halmashauri na GGML lakini kushukuru ni njia ya kuomba tena,msishie hapa, GGML na halmashauri mnapoona fursa kama hizi basi tunaangalia mazingira,kwa kanda hii mazingira yanayoweza kuwa favourable kwa uvuvi ni Nkome,kwahiyo tunaita watu wengi zaidi,tunawakaribisha waje wawekeze,watoe mikopo kwa wana vikundi wanaopatikana katika kata hii,” amesema Kahesi.

Akizungumza wakati wa zoezi la uvunaji wa samaki hao, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Karia Rajab Magaro, amewapongeza wanachama wa kikundi hicho kwa kuonyesha nidhamu, mshikamano na uvumilivu mkubwa katika kipindi chote cha utekelezaji wa mradi.
Amesema mafanikio hayo yanapaswa kuwa mfano kwa vikundi vingine vya uzalishaji katika wilaya hiyo, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kutumia fursa zilizopo kuanzisha miradi yenye tija kwa maendeleo yao na ya jamii kwa ujumla.

"Leo tumekuja kushuhudia matunda ya juhudi zenu kupitia mavuno ya kwanza ya samaki, Nawasihi muendelee kushikamana na kushirikiana ili mradi huu uwe endelevu na uwe mfano kwa vikundi vingine vitakavyonufaika kupitia fedha zitakazorejeshwa kutokana na uwekezaji huu,"
Amesisitiza kuwa Halmashauri ya wilaya ya Geita inaendelea kuwakaribisha wadau mbalimbali wa maendeleo, taasisi za kifedha pamoja na wawekezaji binafsi kuwekeza katika sekta ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba kutokana na uwepo wa rasilimali kubwa ya Ziwa Viktoria ambayo bado ina fursa nyingi za kiuchumi zinazoweza kutumiwa na wananchi.
Mafanikio ya kikundi cha Jiendeleze Mchangani yanaonesha namna ubunifu, ushirikiano kati ya sekta binafsi na jamii, pamoja na uwekezaji katika teknolojia za kisasa za ufugaji wa samaki vinavyoweza kuongeza uzalishaji, kuimarisha kipato cha wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika maeneo yanayozunguka Ziwa Viktoria.
Discussion
Reader comments
0 contributions