Na Ibrahim Rojala - Geita.
Wasamaria wema katika Kitongoji cha Ludete, Kata ya Ludete katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro Mkoani Geita wameokota mtoto mchanga wa kike anayekadiriwa kuzaliwa alfajiri ya siku ya tukio, kisha kutelekezwa katika eneo hilo.
Tukio hilo limebainika baada ya mama mmoja Eunice Mtesigwa, kueleza kuwa wakati akipita katika eneo la tukio, alisikia sauti ya mtoto akilia na kuamua kuifuatilia ndipo alipokikuta kichanga hicho kikiwa kimetelekezwa.

Mama huyo amesema baada ya kumkuta mtoto huyo, alimpatia huduma ya kwanza ikiwemo kumkata kitovu na kumfunika vizuri kabla ya kutoa taarifa kwa uongozi wa serikali ya mtaa.
Muuguzi wa Hospitali ya Katoro, Mussa Alfan amesema mtoto huyo alipokelewa katika hospitali hiyo na kuthibitisha kumpokea mtoto huyo akiwa na uzito wa kilo 2.5 akiwa na hali nzuri na kuanzishiwa matibabu ya antibiotic kwa lengo la kumkinga na magonjwa.

‘Mpaka sasa hali ya mtoto ni nzuri na hana changamoto yoyote,wito wangu kwa wazazi wale ambao hawajiwezi tungeomba waweze kufika kwa viongozi wao ili waweze kupata msaada pale wanapoona kuna changamoto,’ amesema Muuguzi Khalfan.
Akizungumzia hatma ya mtoto huyo, Diwani wa Kata ya Ludete, Jumanne Misungwi ameelezea kuguswa na tukio hilo na kuahidi kumtunza pamoja na kumpatia huduma zote stahiki ikiwa ni pamoja na malezi na elimu,wakati akiendelea na hatua zingine za kumuasili mtoto huyo.

‘Huyu mtoto kuanzia leo ataitwa jina la mama yangu,ataitwa Regina Jumanne,mimi naitwa Jumanne Misungwi na ndio nimesema hata kadi yake iandikwe hivyo na nitamhudumia mpaka mwisho wake atakaposema nimechoka,’ amesema Misungwi
Aidha kufuatia kutokea kwa tukio hilo wakazi wa eneo hilo wamepaza sauti za kukemea matukio ya aina hiyo wakisema ni vyema waanawake kutoa taarifa za changamoto wanazokabiliana nazo kwa viongozi badala ya kufanya maamuzi magumu ya kutupa watoto.
Discussion
Reader comments
0 contributions