Na Saulo Stephen - Singida.
Katibu wa NEC – Oganaizesheni wa Chama Cha Mapinduzi, Issa Ussi Haji maarufu kama Gavu, amewataka madiwani wa CCM mkoani Singida kuwa mstari wa mbele katika kusimamia maendeleo ya wananchi kwa kuhakikisha huduma bora zinawafikia kwa wakati na kwa ufanisi.
Gavu ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na madiwani wa CCM kutoka halmashauri mbalimbali za Mkoa wa Singida katika kikao maalum kilichofanyika mjini Singida.

Katika kikao hicho, amewasisitiza viongozi hao kufanya kazi kwa uadilifu, uwajibikaji na uzalendo wa hali ya juu akieleza kuwa nafasi walizonazo ni dhamana kubwa waliyopewa na wananchi.
Aidha, Gavu amewataka madiwani hao kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za halmashauri wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao, huku akibainisha kuwa wao ni wawakilishi wa wananchi na si watendaji wa halmashauri.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Martha Mlata, aliwaongoza madiwani hao pamoja na Kamati za Siasa za Wilaya na Kamati ya Siasa Mkoa kushiriki kikao hicho muhimu huku akimshukuru Gavu kwa kuzungumzia masuala mbalimbali muhimu yenye lengo la kuimarisha utendaji wa viongozi wa chama na maendeleo ya wananchi.
Katika kikao hicho, madiwani hao pia walipata nafasi ya kujadili changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao na kubadilishana uzoefu wa namna bora ya kuwatumikia wananchi kwa ufanisi zaidi.
Discussion
Reader comments
0 contributions