Wajasiriamali na wafanyabiashara wanaomiliki Kampuni mkoani Geita na nchini kwa ujumla wameshauriwa kujenga uwezo na kujiandaa mapema ili kunufaika na fursa za ajira na zabuni za huduma zinazotokana na kampuni ya uwekezaji wa Anglo Gold Ashanti,(GGML), badala ya kusubiri fursa zitangazwe ndipo waanze maandalizi hayo.
Akizungumza Oktoba 01,2026 kwenye kongamano la kujadili fursa za uwepo wa Mgodi wa GGML kuelekea utekelezaji wa Dira 2050 lililofanyika ukumbi wa Mkapa uliopo viwanja vya maonesho vya Dk Samia Suluhu Hassan Manispaa ya Geita,Afisa manunuzi wa GGML Silas Shija,amesema uwepo wa shughuli za uchimbaji madini mkoani humo,unafungua nafasi kwa wafanyabiashara wa ndani kupitia mnyororo wa thamani.

Afisa Manunuzi wa GGML Silas Shija akiwasilisha mada katika kongamano la kujadili fursa za uwepo wa Mgodi wa GGML kuelekea utekelezaji wa Dira 2050.Picha na Ibrahim Rojala
‘Hutakiwi kusubiri kwamba kazi au tenda zimetoka ndiyo unaanza kujiandaa ili uombe,tunashauri Kampuni za kizawa zijiandae kabla,kuliko kusubiri ikitokea fursa ndipo zianze kujiandaa”.
Shija amesema kampuni ambazo tayari zimesajiliwa zinapaswa kufuatilia matangazo ya zabuni na ajira yanayotolewa kupitia magazeti na njia nyingine rasmi ili kutumia fursa hizo na kueleza kuwa serikali ina wajibu wa kuhakikisha mwekezaji na kampuni za kizawa wanapata mazingira yanayowawezesha kushiriki katika fursa za kiuchumi kupitia sheria na kanuni zilizo wazi.
Akizungumzia namna Mgodi huo umejiandaa kuwezesha ufikiwaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 20250 ameeleza kuwa asilimia 95% yamalipo yaliyofanywa na kampuni hiyo yalifanywa kwa kampuni za ndani wakatiasilimia 90 ya Huduma zilizotolewa ndani ya mgodi huo zilitolewa na kampuni zilizosajiliwa Tanzania.
Aidha zaidi ya wajasiriamali 300 kutoka mkoani Geita wamepatiwa mafunzo ya sheria, kanuni, miongozo na taratibu maalum za manunuzi na uwepo wa miradi 61 ya kijamii inayotekelezwa kupitia CSR.
Akizungumza kwenye kongamano hilo,Meneja wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii NSSF Mkoa wa Geita, Winniel Lusingu,amesema licha ya utayari wanaotakiwa kuwanao wananchi kuhusu fursa hizo,ametoa rai kwa GGML kuwekeza pia kwenye utoaji elimu ili jamii iweze kuwa na uwezo wa kujisimamia.

Meneja wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii NSSF Mkoa wa Geita, Winniel Lusingu akiwasilisha mada mada katika kongamano la kujadili fursa za uwepo wa Mgodi wa GGML kuelekea utekelezaji wa Dira 2050.Picha na Ibrahim Rojala
"Kuwapa elimu si lazima kifedha lakini kuwpaa uwezo wa wao kuweza kujisimamia itawaongeza kwenye idadi ya watu ambao wako rasmi lakini itaongeza kipato kwa wananchi".
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Uendelevu na Mahusiano ya Jamii wa Mgodi wa GGML,Gilbert Mworia amesema kampuni hiyo imekuwa na mchango katika maendeleo ya jamii kupitia ulipaji kodi na uwekezaji katika sekta mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara, huduma za afya, elimu na uwekezaji katika kilimo ni miongoni mwa maeneo ambayo kampuni imekuwa ikichangia kama sehemu ya wajibu wake kwa jamii.“Tunao wajibu kwa jamii inayotuzunguka ili tuendelee kupata ridhaa ya wananchi kuendelea kufanya shughuli zetu,sisi kama kampuni huwa tunarudisha fadhila kwa jamii inayotuzunguka, si Geita tu bali maeneo mbalimbali nchini,” amesema Gilbert

Mkurugenzi wa Usimamizi wa Uendelevu na Mahusiano ya Jamii wa Mgodi wa GGML,Gilbert Mworia akizungumzia mchango wa kampuni hiyo katika maendeleo ya Jamii kupitia kongamano la kujadili fursa za uwepo wa Mgodi wa GGML kuelekea utekelezaji wa Dira 2050.
Mworia amesema kwa Halmashauri ya Wilaya ya Geita na Manispaa ya Geita, kampuni hiyo hutenga Sh9.2 bilioni kila mwaka kwa ajili ya miradi katika sekta za Elimu, Afya, Miundombinu, Barabara na maji katika kipindi ambacho GGML pia hutumia kati ya Shilingi Bilioni 13 hadi Shilingi Bilioni 15 kwa mwaka kufadhili Taasisi, Mashirika, Serikali na watu binafsi katika maeneo mbalimbali.
Ametaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni ushirikiano na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), ambapo kampuni hiyo imeingia mkataba wa miaka mitatu wa kusaidia watoto wenye matatizo ya moyo.
Aidha, amesema kampuni hiyo ina meli ya huduma za afya inayotoa huduma kwa wananchi wanaoishi katika visiwa 10 vya Ziwa Victoria, hususan katika mikoa ya Geita, Mwanza na Kagera ujenzi wa madarasa 1,000, vituo vya afya na zahanati zaidi ya 150 pamoja na kuchangia ujenzi na uboreshaji wa hospitali.

Baadhi ya washiriki wa kongamano la kujadili fursa za uwepo wa Mgodi wa GGML kuelekea utekelezaji wa Dira 2050.
Baadhi ya wajasiriamali,wachimbaji na wadau wa sekta ya uchimbaji walioshiriki kongamano hilo,wameomba kupatiwa elimu zaidi namna ya kuomba tenda pindi zinapotangazwa ili kunufaika na fursa zinazotolewa na mgodi huo.
Kongamano hilo limefanyika ikiwa ni maadhimisho ya tisa ya teknolojia ya madini,yenye kaulimbiu isemayo Madini ni Utajirituwajibike kwa Pamoja Kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050”,ambapo mgodi huo umedhamiria kushiriki kufikia malengo hayo huku Serikali ikitegemea sekta binafsi kwa asilimia 70.
Discussion
Reader comments
0 contributions