Serikali imeendelea kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika utoaji wa huduma kwa wananchi, ambapo sasa Watanzania wasio na vyeti vya kuzaliwa watanufaika na Mfumo wa Kidijitali wa eRITA unaowezesha upatikanaji wa vyeti hivyo ndani ya saa 48.
Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Juma Zuberi Homera, amesema hayo alipotembelea Banda la Wizara hiyo, katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).

Amesema mfumo wa eRITA ni sehemu ya mageuzi ya Serikali ya kidijitali yanayolenga kurahisisha na kuharakisha utoaji wa huduma muhimu kwa wananchi, huku ukiongeza ufanisi na uwazi.
“Mfumo wa Kidijitali wa eRITA umekuwa mfumo bora kabisa katika taasisi hii kwani utarahisisha upatikanaji wa vyeti vya kuzaliwa. Badala ya kusubiri kwa muda mrefu, sasa mwananchi anaweza kupata cheti chake ndani ya saa 48,” amesema Dkt. Homera.

Pia, amewahimiza Watanzania kutembelea banda la Wizara ya Katiba na Sheria katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) ili kupata huduma mbalimbali za kisheria na usajili wa vizazi na vifo.
"Baada ya kutembelea banda letu, wananchi watapata msaada wa kisheria, ushauri wa kitaalamu na kuelekezwa namna ya kushughulikia changamoto zao za kisheria, ikiwemo kupatiwa wakili pale inapohitajika," amesema.

Ameongeza kuwa Wizara ya Katiba na Sheria imejipanga kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa urahisi, huku akipongeza Katibu Mkuu wa wizara hiyo na wataalamu kwa maandalizi mazuri ya banda hilo katika maonesho ya mwaka huu.

Discussion
Reader comments
0 contributions