Na Gideon Gregory - Dodoma.
Kutokana na watu wengi wenye elimu na hata vipato vya uhakika kukumbwa na changamoto za kukosa nidhamu ya matumizi ya fedha, Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM), imependekeza elimu ya usimamizi wa fedha ianze kutolewa kwa watoto tangu wakiwa shule za awali.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Agosti 6,2026 Jijini Dodoma Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dkt. Maulid Maulid amesema changamoto ya financial literacy au elimu ya usimamizi wa fedha siyo kwa watu wasio na elimu pekee, bali hata kwa wasomi na wataalamu wanaoshindwa kupanga matumizi ya fedha walizonazo hadi kukamilisha mahitaji yao ya kila mwezi.
"Hali hiyo imechangia baadhi ya watu kuingia kwenye madeni makubwa na kukopa zaidi ya uwezo wao wa kulipa, jambo linaloonyesha umuhimu wa kuwajengea watoto uelewa wa nidhamu ya fedha mapema wakiwa bado wadogo," amesema.
Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dkt. Maulid Maulid.
Kwa mujibu wa ADEM, suluhisho la muda mrefu ni kuingiza maarifa ya usimamizi wa fedha kwenye mitaala ya viongozi wa elimu ili wanaposimamia shule waweze kuhakikisha wanafunzi wanafundishwa stadi za kupanga bajeti, kutumia fedha kwa uangalifu, kuweka akiba na kufanya maamuzi sahihi ya kifedha.
Mtendaji huyo amesema lengo ni kuwajengea wanafunzi uwezo wa kusimamia rasilimali walizonazo tangu ngazi ya elimu ya awali, msingi hadi sekondari, ili wanapofikia utu uzima wawe na utamaduni wa matumizi yenye tija badala ya kutegemea mikopo isiyoendana na uwezo wao.
Katika hatua nyingine Dkt. Maulid amesema kwa zaidi ya miaka 25 ya utekelezaji wa majukumu yake, ADEM imekuwa ikitoa mchango mkubwa katika kuandaa viongozi wenye uwezo wa kusimamia mabadiliko na kusaidia Serikali kufikia malengo ya kujenga mfumo bora wa elimu nchini.
“Uongozi bora wa elimu ni msingi wa kujenga mfumo wa elimu unaozalisha wataalamu wenye maarifa, ujuzi na ubunifu unaohitajika katika maendeleo ya Taifa,” amesema Dkt. Maulid.
Ameeleza kuwa ADEM, ambayo ipo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imeendelea kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) katika kuwafikia viongozi wa elimu kuanzia ngazi ya shule hadi mikoa.
Taasisi hiyo kwasasa inalenga kuwa kituo kinachoongoza katika maendeleo ya uongozi wa elimu barani Afrika na kuchangia kujenga mfumo wa elimu utakaowezesha Tanzania kupata wataalamu wenye uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.
Discussion
Reader comments
0 contributions