Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Upendo Wella, ameongoza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya (KUU) kutembelea Bwawa la Italiano lililopo Mtaa wa Ikindwa, Kata ya Mapambano, kwa lengo la kujionea hali ya bwawa hilo na kutathmini hatua za tahadhari za kuchukua kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Bi Upendo Wella amesema kuwa wamefika eneo hilo pamoja na wataalamu kwa ajili ya kujionea hali halisi na kuweka mikakati ya kujiandaa kukabiliana na mvua hizo, kufuatia utabiri wa mamlaka husika kuhusu uwezekano wa baadhi ya mikoa nchini kukumbwa na mvua za El Niño.
Amesema Wilaya ya Tabora imeendelea kuchukua hatua za tahadhari kwa kutembelea maeneo mbalimbali ili kubaini changamoto zinazoweza kujitokeza na kuweka mikakati ya kukabiliana nazo mapema.
Aidha, DC Wella amewataka wananchi wa Wilaya ya Tabora kuendelea kupokea na kufanyia kazi elimu na tahadhari zinazotolewa na wataalamu kupitia mikutano na kampeni zinazoendelea katika mitaa na kata mbalimbali wilayani humo.
Amewasisitiza wananchi kuhakikisha wanatunza usafi wa mazingira kwa kufukua na kusafisha mitaro ya maji, kuondoa vizuizi vinavyoweza kuzuia mtiririko wa maji na kuhakikisha maeneo yao yanakuwa salama ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Wilaya ya Tabora katika kuimarisha maandalizi na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu namna ya kujikinga na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño.
Discussion
Reader comments
0 contributions