Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Bi. Upendo Joseph Haule, akimwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora amefungua rasmi kikao cha utambulisho wa Mradi wa America First Global Health Strategy (AFGHS) unaotekelezwa na Shirika la Elizabeth Glaser Pediatric AIDS Foundation (EGPAF) mkoani Tabora ambapo kikao hicho kimefanyika katika Ukumbi wa Mtemi Isike Mwanakiyungi Manispaa ya Tabora. 
Katibu wa Afya Mkoa wa Tabora, Bw. Joseph Mwanambesi, akimwakilisha Mganga Mkuu wa Mkoa, amesema kikao hicho kimeitishwa baada ya kukamilika kwa Mradi wa Afya Jumuishi uliotekelezwa na MDH, ili kuitambulisha EGPAF kama mshirika mpya na kuimarisha ushirikiano wa Serikali na wadau katika afua za VVU/UKIMWI.
Bi. Haule ameishukuru MDH kwa mchango wake katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za VVU/UKIMWI mkoani Tabora na kuipongeza EGPAF kwa kuanza utekelezaji wa mradi huo.
Amehimiza ushirikiano huo uendelee na kuimarishwa zaidi, akisema bado kuna kazi kubwa katika mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI.
Aidha Bi. Haule amesema mkoa una vituo 460 vya kutolea huduma za afya, ambapo vituo 254 vinatoa huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU. Kati ya hivyo, vituo 167 vilikuwa vikipata ufadhili kupitia mradi uliokamilika. 
Ameitaka timu ya afya ya Mkoa, kwa kushirikiana na Halmashauri, kutathmini mgawanyo wa huduma na kubaini mapengo.
Pia amesisitiza umuhimu wa mwendelezo wa matibabu, huduma kwa watoto na vijana, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, na matumizi ya takwimu kuboresha huduma.
Mkurugenzi wa EGPAF nchini, Dkt. Sajida Kimambo, amesema Mradi wa AFGHS ulianza kazi Septemba 2026 na itaunga mkono huduma za VVU, kifua kikuu na juhudi za kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, huku akisema vipaumbele vyake ni kuimarisha uongozi wa Serikali, kutoa huduma zinazomweka mteja mbele.
Kwa upande wake mratibu wa Mradi wa MDH mkoani Tabora, Dkt. Nicholaus Tarimo, amesema mafanikio yaliyopatikana yametokana na utayari na ushirikiano kati ya MDH na Serikali, pamoja na matumizi sahihi ya rasilimali zilizotolewa na Serikali ya Marekani.
Discussion
Reader comments
0 contributions