Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Dkt. John Pima, ameshuhudia hafla ya utiaji saini wa mkataba wa ruzuku yenye thamani ya Dola za Marekani 111,758 kutoka Serikali ya Japan kwa ajili ya kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto katika Manispaa ya Tabora.
Ruzuku hiyo imetolewa kupitia Mpango wa Msaada wa Ruzuku kwa Miradi ya Usalama wa Binadamu ya Ngazi ya Jamii (Grassroots Human Security Projects), ikiwa na lengo la kuimarisha upatikanaji wa vifaa muhimu vya huduma za afya ya watoto wachanga, wajawazito na wanawake baada ya kujifungua.
Kupitia mradi huo, wananchi wanaopata huduma katika Hospitali ya Misheni ya Mtakatifu Anna (St. Ann) iliyopo Kata ya Ipuli, AMUCTA iliyopo Kata ya Kanyenye na Zahanati ya Kipalapala iliyopo Kata ya Itetemia wanatarajiwa kunufaika na kuboreshwa kwa upatikanaji wa vifaa vya matibabu, hatua itakayochangia kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto na kupunguza hatari zinazoweza kujitokeza wakati wa ujauzito, kujifungua na siku za mwanzo za maisha ya mtoto.
Akizungumza katika hafla hiyo, ujumbe wa shukrani kwa niaba ya Halmashauri ya Manispaa ya Tabora umetambua mchango wa Serikali ya Japan na wananchi wake katika kuunga mkono juhudi za kuboresha huduma za afya nchini Tanzania.
Aidha, akizungumza katika hafla hiyo Askofu msaidizi wa Jimbo kuu katoliki Tabora Mhashamu Josaphat Bududu amesema kuwa ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za afya za kidini na washirika wa maendeleo ni muhimu katika kuboresha huduma za kijamii na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na salama za afya.
Halmashauri ya Manispaa ya Tabora imejipanga kushirikiana na taasisi zinazohusika kuhakikisha vifaa vitakavyopatikana kupitia mradi huo vinatumika ipasavyo, vinatunzwa na kuleta manufaa endelevu kwa wananchi.
Mradi huo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Japan katika kuboresha huduma za afya na kulinda maisha ya akina mama na watoto wachanga.
Discussion
Reader comments
0 contributions