Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt. John Mboya, amewataka washiriki wa mafunzo ya utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Programu ya SCALE kutumia maarifa waliyoyapata kuibua na kutekeleza miradi inayolenga kutatua changamoto halisi za wananchi, hususan zinazohusiana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Dkt. John Mboya ametoa wito huo wakati akifunga rasmi mafunzo ya siku nne yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mtemi Isike Mwanakiyungi, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora.
Mafunzo hayo yamewashirikisha watendaji kutoka Halmashauri za Wilaya za Igunga na Nzega pamoja na timu za uratibu wa Programu ya SCALE, kwa lengo la kuwawezesha washiriki kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa programu hiyo katika awamu ya pili.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Dkt. Mboya amesema ushiriki wa wananchi ni msingi muhimu wa mafanikio ya programu, akisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kushirikishwa katika kutambua changamoto, kupanga vipaumbele na kufuatilia utekelezaji wa miradi inayotekelezwa katika maeneo yao.
Amesisitiza kuwa mahitaji na vipaumbele vitakavyobainishwa na wananchi vinapaswa kuingizwa katika mipango na bajeti za halmashauri ili kuwezesha utekelezaji wa miradi yenye tija na matokeo yanayoonekana katika jamii.
“Katika awamu hii, mafanikio yetu hayapaswi kupimwa tu kwa idadi ya Kata au jamii zilizofikiwa, bali pia kwa ubora wa ushiriki wa wananchi na kiwango ambacho vipaumbele vyao vinaonekana katika mipango, bajeti na utekelezaji wa shughuli za maendeleo,” amesema Dkt. Mboya.
Akizungumzia utekelezaji wa Awamu ya Kwanza ya Programu ya SCALE, Dkt. Mboya amesema jumla ya miradi 24 ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ilikidhi vigezo vya Benki ya Dunia na kutengewa zaidi ya shilingi bilioni 1.36.
Amesema kati ya miradi hiyo, miradi 12 inatekelezwa katika kata 12 za Halmashauri ya Wilaya ya Igunga, ikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 681, huku miradi mingine 12 ikiwa katika kata 12 za Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, yenye thamani zaidi ya shilingi 684.
Kwa mujibu wa Dkt. Mboya, uzoefu uliopatikana katika awamu ya kwanza unapaswa kuwa msingi wa kuboresha uhamasishaji, uwezeshaji na uratibu wa shughuli katika Awamu ya Pili ya programu hiyo.
Katika hatua nyingine Dkt. John Mboya amewataka watendaji wa Halmashauri za Igunga na Nzega kuhakikisha miradi inayotekelezwa inasimamiwa kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyowekwa.
Aidha, amewataka kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na kuwasilisha taarifa za utekelezaji kila mwezi, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia hatua stahiki za kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua wakati wa utekelezaji wa miradi.
Amewataka pia washiriki wa mafunzo hayo kutumia ujuzi na uzoefu walioupata katika kuimarisha utekelezaji wa shughuli za programu, pamoja na kuwasilisha taarifa baada ya kukamilisha kazi za uwandani.
Discussion
Reader comments
0 contributions