Na Saulo Stephen - Singida.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga, ameongoza timu ya wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kufanya ufuatiliaji wa hali ya ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri ya Manispaa ya Singida, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha halmashauri hiyo inafikia malengo ya makusanyo yaliyowekwa na Serikali.
Akizungumza na maafisa wa halmashauri hiyo wakati wa ziara hiyo, Dk. Mganga alisema lengo la ufuatiliaji huo ni kutathmini mwenendo wa ukusanyaji wa mapato, kubaini changamoto zinazojitokeza na kuweka mikakati ya kuongeza ufanisi katika makusanyo ya mapato ya ndani.

Alieleza kuwa mapato ya ndani yana mchango mkubwa katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo na utoaji wa huduma muhimu kwa wananchi, ikiwemo sekta za elimu, afya, maji, usafi wa mazingira pamoja na ujenzi wa miundombinu.
“Ukusanyaji mzuri wa mapato huongeza uwezo wa halmashauri kugharamia miradi ya maendeleo na kuboresha huduma kwa wananchi, huku ukipunguza utegemezi wa ruzuku kutoka Serikali Kuu,” alisema Dk. Mganga.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa usimamizi madhubuti wa mapato, akibainisha kuwa ni msingi muhimu wa kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii pamoja na ustawi wa wananchi wa Manispaa ya Singida.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuongeza uwezo wa mamlaka za serikali za mitaa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuharakisha maendeleo ya wananchi.

Discussion
Reader comments
0 contributions