Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Dkt. Fatuma Mganga, ametoa wito kwa wananchi na wafanyabiashara mkoani humo kujisajili na Shirika la Bima la Taifa (NIC) kwa kukata bima, kama mkakati wa kujikinga dhidi ya changamoto na majanga yasiyotarajiwa.
Wito huo umetolewa leo Oktoba 5, 2026 wakati akizindua kampeni ya maonesho ya barabarani na utoaji wa elimu ya bima kwa jamii iitwayo ‘NIC Kitaa’, iliyoandaliwa na Shirika la Bima la Taifa (NIC) yenye lengo la kutoa elimu ya bima kwa wananchi wa mkoa huo.

Dkt. Fatuma amesema majanga kama vile moto na mvua za juu ya wastani zinazotarajiwa mapema mwezi huu yamekua na athari kubwa nchini, hivyo ni muhimu kwa jamii kukata bima ili kukabiliana nayo na mfanyabiashara anapaswa kuwa nayo ili kulinda biashara zao.
Vilevile, ameliipongeza NIC kwa kazi nzuri ya utoaji wa bima na kwa kuanzisha kampeni hiyo muhimu ambayo itasaidia wananchi wengi kuwa na bima katika vyombo vyao vya usafiri, biashara na nyumba.

Kwa upande wake, Meneja wa Shirika la Bima la Taifa Kanda ya Ziwa, Bi. Stella Marwa, ametumia fursa hiyo kuomba ushirikiano kutoka kwa taasisi nyingine za serikali kama za kifedha na Jeshi la Polisi katika kutoa elimu ya bima kwa wananchi ndani ya mkoa huo ili waweze kujiunga na huduma hiyo.

Discussion
Reader comments
0 contributions