Na Saulo Stephen – Singida.
Mkuu wa Divisheni ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii Manispaa ya Singida, Dkt. Geofrey Andrew, amesisitiza umuhimu wa lishe bora kwa watoto, akieleza kuwa lishe yenye uwiano ni msingi muhimu katika kuboresha afya, ukuaji na uwezo wa watoto kujifunza na kufanya vizuri shuleni.
Dkt. Andrew ameyasema hayo wakati akiongoza Kikao cha Lishe cha Robo ya Nne kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida, Bi. Joanfaith Kataraia, kilichofanyika katika Ukumbi Mdogo wa Mkurugenzi, Ofisi za Manispaa ya Singida.

Amesema kuhakikisha watoto wanapata lishe bora kunapaswa kuwa jukumu la pamoja la familia, jamii na Serikali, kwa kuwa hali ya lishe ya mtoto ina mchango mkubwa katika ukuaji wake kimwili na kiakili pamoja na maendeleo yake kitaaluma.
Kwa mujibu wa Dkt. Andrew, watoto wanaopata lishe bora huwa na afya njema, uwezo mzuri wa kujifunza na kushiriki kikamilifu katika shughuli za shule na jamii.
Kikao hicho pia kililenga kupitia utekelezaji wa shughuli mbalimbali za lishe katika Manispaa ya Singida, kubaini changamoto zilizopo na kuweka mikakati ya kuboresha hali ya lishe kwa watoto.

Aidha, kikao hicho kimekuwa sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Serikali yanayolenga kuhakikisha watoto wanakuwa na afya bora na mazingira wezeshi ya kujifunza ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao.
Dkt. Andrew amesisitiza kuwa juhudi za kuboresha lishe kwa watoto zinapaswa kuendelea kupewa kipaumbele ili kujenga kizazi chenye afya, uwezo wa kujifunza na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya Taifa.
Discussion
Reader comments
0 contributions