Ikiwa ni siku chache tangu Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kutoa tahadhari ya uwepo wa mvua za El nino,diwani wa kata ya Majengo Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga Zacharia Soko ameamua kujenga mitaro ya kupitisha maji kwa gharama zake ili kukabiliana na mvua za Eli nino zinazotarajiwa kunyesha hivi karibuni.
Akizungumza na waandishi wa habari amesema kuwa katika kutimiza hilo atatumia kiasi cha Shilingi milioni sita kwa ajili ya mitaro na makalavati ili kuepusha kata yake ambayo iko eneola bondeni kukumbwa na mafuriko wakati wa mvua hizo.
“Kata ya majengo ipo bondeni kijographia na mvua zote zinaponyesha kutoka kata za Nyahanga,Nyasubi na Kahama mjini maji yote yanakuja kata ya Majengo sasa kutokana na hali ya hewa ya mwaka huu tunatakiwa tujipange ili kukabiliana na mafuriko ndiyo maana nimeamua kutenga kiasi cha shilingi milioni sita ili kukarabati mitaro na makaravati ya maji” amesema Soko.
Mbali na ujenzi wa mitaro na makaravati Soko amechonga baadhi ya barabara za ndani ya kata ambazo zimekuwa na usumbufu wa kupitika mara kwa mara zikiwemo za Sokola,Majani mapana pamoja na stendi ndogo ili ziweze kutumika wakati wote hata wa masika.
“Mitaro na makaravati pekee si kitu kama hatujaziboresha barabara zetu kwahiyo sambamba na mitaro hii pia tutarekebisha barabara zote korofi ili ziweze kupitika muda wote,tumechonga barabara za mitaa ya Sokola,Majani mapana na zingine ambazo ni mbovu ili ziweze kupitika wakati wote hususan kuelekea kwenye kipindi cha mvua” Ameongeza .
Katika hatua nyingine amewataka wakazi wa kata ya Majengo kuacha tabia ya kutupa taka kwenye mitaro kwani inasababisha mifereji kuziba na matokeo yake maji kukosa uelekeo na kuleta mafuriko.
“Niwaombe sana wananchi wa Majengo tuache tabia ya kutupa taka ngumu kwenye mitaro kwani inasababisha maji kukosa uelekeo sisi kata yetu ipo mabondeni sasa tunapoziba mitaro tunasababisha maji kukosa uelekeo na kupata mafuriko” Amesisistiza Soko.
Msimamizi wa mradi huo Jafari Kingu amesema mradi huo utakamilika kwa wakati, huku baadhi ya wakazi wa kata hiyo Ansela Mkono na Richard Mutatina wakimpongeza hatua ya diwani huyo.
“Sisi tumejipanga vizuri kuhakikisha tunamliza ujenzi huu ndani ya Muda,niwaombe wananchi watupe ushirikiano ili tukamilishe kwa wakati,tunamshukuru sana Mh Diwani kwa kujitoa sana katika miradi ya kusaidia wananchi kwakweli miundombinu yetu ilikuwa si rafiki lakini ametusaidia kwa kiasi kikubwa kutatua kero za barabara” Amesema injiania Kingu na wananchi wa Majengo.
Discussion
Reader comments
0 contributions