Aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda ametumia mistari ya biblia kumkabidhi ofisi mrithi wake Dkt. Francis Mlacha ikiwa ni msisitizo wa kuweka nguvu katika kulinda haki za wananchi na kukabiliana na uonevu.
Makabidhiano hayo, yamefanyika Oktoba 6,2026 baada ya Nkinda Kuhamishwa na kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mkoani Singida, huku Dkt. Mlacha akiteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga.
Akitumia kitabu cha Mithali 31:8-9 inayowataka viongozi kuwatetea wasiojiweza na kuwapatia haki maskini na wahitaji Nkinda amesisitiza kuhusu watu wa tabaka la chini ambao hawana watu wa kuwasemea huku akirejea kitabu cha Isaya1:17 anaosisitiza Kutenda mema kutafuta haki na kuwasaidia wanaoonewa.
“Nikukaribishe sana Wilayani Kahama Mh Mkuu wa wilaya,Kahama ni shwari na salama na wananchi wako imara wanachapa kazi,kikubwa nikuombe kuzidi kuwatetea wananchi wanyonge wa Kahama,Asilimia kubwa ya watu wenye fedha Kahama wanaamini Fedha kuliko haki za wanyonge,kilio kikubwa cha wanyonge wa Kahama ni suala la kukosa haki na hawana furaha Mungu akusaidie tunakuombea ushinde katika hili” Amesema Nkinda.

Sambamba na hayo Nkinda amemtaka Dkt. Mlacha kutumia nafasi yake kusimamia haki akirejea mafundisho ya biblia yanayosisitiza viongozi kufungua vinywa vyao kwa ajili ya wasio na uwezo wa kujitetea.
“Maandiko yanatutaka sisi viongozi kufungua vinywa vyetu kuwasemea wasio na uwezo wa kusema,wapo watu ambao kwa nafasi zao wana uwezo wa kusema na wana uwezo wa kumfikia yeyote ila wapo ambao nafasi hiyo hawana na hawajui waanzie wapi hivyo ni vyema kwa nafasi yako ukawasemea watu hawa ili wapate haki zao.” Ameongeza Nkinda.
Mbali na suala la haki,Nkinda amemtaka mkuu huyo wa wilaya kuwa tayari kukabiliana na changamoto ya wizi wa mita za maji ambao umedumu kwa zaidi ya mwaka mmoja kabla ya kudhibiti wizi huo baada ya kuwakamata baadhi ya wahusika huku uchunguzi ukionyesha kulikuwa na watu wenye ushawishi waliokuwa nyuma ya wizi huo.
“Nilipokuja Kahama Changamoto ya wizi wa mita za maji ilikuwa na miezi kumi nyuma bila Ufumbuzi,Tulipambana na tukawakamata wahalifu lakini tukagundua kulikuwa na watu wakubwa wenye ushawishi nyuma ya wizi huu,Hivyo hili nalo ukae nalo macho.” Amesisitiza Nkinda。

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kahama ambaye anachukua nafasi ya Nkinda, Dkt. Francis Mlacha ameshukuru kwa makaribiso hayo na amehaidi kushirikiana na wananchi wa wilaya ya Kahama na kuzingatia yote ambayo mtangulizi wake amemwambia.
“Nimekaribia Kahama na ninamshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuniamini na kuniteuwa kuwa mkuu wa wilaya ya Kahama,Nitashirikiana na wananchi Pamoja na watumishi wenzangu wa wilaya ya Kahama ili kuhakikisha Kahama ina songa mbele na nitazingatia yote ambayo mtagulizi wangu amenieleza” Amesema Mlacha.

Discussion
Reader comments
0 contributions