Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mhe. Johari Samizi amekabidhi Pikipiki 11 kwa Maafisa Afya wa kata kutokana na ufaulu wa mradi na kuwataka kuzitumia pikipiki hizo kuimarisha uhamasishaji na ukaguzi wa usafi wa mazingira katika jamii.
Amekabidhi pikipiki hizo Tarehe 22 Septemba 2026 baada ya kikao cha utekelezaji wa kampeni ya usafi wa Mazingira kilichofanyika Aprili hadi Septemba 2026 ambapo pia amewataka watendaji wa Kata na Vijiji kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, kanuni pamoja na utekelezaji wa Sheria ndogo za usafi wa Mazingira ili kuendelea kuimarisha hali ya afya na usafi wa Mazingira.
Akiwasilisha Taarifa ya utekelezaji wa kampeni ya usafi wa Mazingira wa mwezi Aprili hadi Septemba 2026 Afisa Afya wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Ivona Mabala amesema kuwa vituo 21 vimebainishwa kwa ajili ya maandalizi na kuwasilishwa katika uhakiki wa usafi wa mazingira ambapo pia vyoo bora vimeongezeka kutoka asilimia 65.05 mwezi Machi 2026 hadi kufikia asilimia 71.37 kwa mwezi Juni 2026 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 6.34.
Aidha katika kipindi hicho kaya zisizo na vyoo zimepungua kutoka asilimia 4.67 hadi asilimia 4.03 sawa na upungufu wa asilimia 0.64
Katika hatua nyingine Kaimu Mkuu wa kitengo cha huduma ya udhibiti wa taka na Usafishaji wa Wilaya hiyo Abubakar Abdallah amesema kuwa ongezeko la uondoshaji wa taka kutoka katika maeneo ya Umma yakiwemo ya Masoko, Vituo vya mabasi, Magulio na Minada kutoka asilimia 15 kuanzia mwezi Julai 2025 hadi asilimia 75 kwa mwezi Julai 2026 .
"Hatua hiyo imeongeza makusanyo ya ada ya uondoshaji wa taka na kuongeza wigo wa utoaji wa huduma kutoka Kata Moja hadi kufikia kata ya pili.Alisema
Mkuu wa Taasisi ya Kuazuia na Kupmbana na Rushwa(TAKUKURU) Wilaya ya Misungwi, Elly Makala amewasisitiza watendaji kuendelea kuwepo katika ofisi zao ili kutoa huduma kwa Wananchi.
Discussion
Reader comments
0 contributions